1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern wawabomoa Bochum, wapinzani wateleza

Bruce Amani
22 Agosti 2022

Ni wazi Bayern Munich hawajamkosa kabisa Robert Lewandowski. Sadio Mane alifunga mabao mawili zaidi na Bayern ikalipiza kisasi cha kichapo cha nadra kilichotokea msimu uliopita kwa kuirindima tena Bochum 7 - 0

https://p.dw.com/p/4FsX9
Fußball Bundesliga | VfL Bochum - FC Bayern München
Picha: Neundorf/Kirchner-Media/IMAGO

Mane sasa ametikisa nyavu mara tatu tangu alipohamia Allianz Arena akitokea Liverpool.

Mwanzo mbaya wa Eintracht Frankfurt uliendelea baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Cologne. Frankfurt ambao watacheza katika Champions League msimu huu kwa mara ya kwanza tangu waliposhindwa katika fainali ya Kombe la Ulaya la 1960 dhidi ya Real Madrid, wana pointi mbili sasa kutoka kwa mechi zao tatu za ufunguzi katika Bundesliga.

Fussball Bundesliga | BVB Dortmund - Werder Bremen
Modeste alipata wakati mgumu katika ushambuliajiPicha: Laci Perenyi/IMAGO

Mchezo ulioshangaza sana hata hivyo ni uliotokea katika dimba la Signal Iduna Park. Werder Bremen walipambana kutokea nyuma mabao mawili kwa sifuri katika dakika ya 89 na kupata ushindi wa ajabu wa 3-2 dhidi ya Borussia Dortmund. Ni mechi ambayo tulikuletea LIVe. B

RB Leipzig bado inatafuta ushindi katika msimu huu baada ya kupata kipigo cha uchungu cha 2 -1 ugenini dhidi ya Union Berlin. Wageni Leipzig walicheza vizuri  na kuumiliki mpira kwa asilimia kubwa lakini wakaambulia patupu.

Jinamizi la mwanzo mbaya wa msimu limeendelea kuikumba Bayer Leverkusen baada ya kuzabwa 3-0 na Hoffenheim. Leverkusen ambao walipigiwa upatu kufanya vizuri msimu huu sasa wanashika mkia bila pointi hata moja. Kwingineko, Freiburg ilipata ushindi wa 1 – 0 dhidi ya Stuttgart wakati Mainz ikiishinda Augsburg 2 -1. Schalke walipata pointi muhimu katika sare ya 0-0 dhidi ya Wolfsburg.

afp