Bayern Munich yailaza Schalke 2:0 | Michezo | DW | 02.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Bayern Munich yailaza Schalke 2:0

Oliver Kahn kustaafu kabisa Juni mwakani.Ronaldinho avuna sasa fedha nyingi zaidi kumpita Beckham.

Roy Makaay aifumania Schalke kwa bao lake la 100

Roy Makaay aifumania Schalke kwa bao lake la 100

Bayern Munich, yailaza Schalke- viongozi wa Bundesliga mabao 2:0 na matumaini yake ya ubingwa yafufuka tena.Oliver Kahn, kipa wa Taifa aliestaafu baada ya kombe la dunia lililopita, athibitisha atstaafu kabisa mwishoni mwa msimu ujao.Young Africans ya Tanzania, yafunga safari ya Tunisia kwa changamoto ya ijumaa hii ya kombe la klabu bingwa barani Afrika.

Kesho ni zamu tena ya champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya-Bayern munich yaumana na AC Milan ya Itali.

Na Ronaldinho wa Brazil, ampiku David Beckham wa Uingereza kuwa mchezaji dimba anaelipwa bora kabisa duniani.Hayo na mengineo, ndio nilio waandalia jioni hii:

Kufuatia changamoto za mwishoni mwa wiki,mabingwa wa Ujerumani-Bayern Munich wamefufua matumaini yao ya kuweza kutwaa ubingwa baada ya viongozi wa Ligi-Schalke kuzabwa mabao 2:0 katika allianz Arena na kuacha pointi 3 nyengine.

Roy Makay aliufumania mlango wa Schalke kwa bao lake la 100 kwa Bayern Munich.Ushindi huo umeiweka Munich pointi 6 tu kutoka Schalke ilipo na wengi sasa wameanza kuipigia tena upatu bayern Munich kwamba ikikaza kamba yaweza mwishoe kulitia tena taji mfukoni ambalo wengi walikwishakata tama kwamba wangetoka msimu huu mikono mitupu.

Kocha wa Bayern Munich, Ottmar Hitzfeld hataki kuzungumzia ubingwa wakati huu.Kinachomsumbua ni tikiti kwa Bayern munich kuweza msimu ujao kucheza katika Champions League-kombe la klabu bingwa barani ulaya.Ikijikuta Munich sasa nafasi ya 4 nyuma ya Schalke,Bremen na Stuttgart,Munich lazima iipiku Stuttgart ili kucheza katika Champions League na baadae jkuanza kuota ndoto ya ubingwa mwenginewa Bundesliga.Hitzfeld anasema:

“Tena na tena yazungumzwa sasa Bayern munich kunyakua ubingwa.Mimi kinachonishughulisha zaidi wakati huu ni kutekeleza jukumu la kwanza kabisa nalo kuipatia Bayern munich ticket ya Champions League-kwani hatukuitia mfukoni.”

Nae kipa wa Bayern Munich,aliekua pia kipa wa Taifa na kipa bora duniani –Oliver Kahn, amethibitisha jana kwamba msimu ujao utakuwa wa mwisho kwake kulinda lango.

Anapanga kustaafu Juni 2008.Mwenyekiti wa Bayern munich,Karl-heinz rumme nigge,alijaribu mwezi uliopita kumshawishi Oliver Kahn kubadili maoni yake na kutia saini mkataba mpya.Alikataa.

Katika Premier League-Ligi ya Uingereza,Manchester united iliikandika Blackburn mabao 4-1 na Chelsea ilitia bao la dakika za mwisho huko Watford na kuifanya Ligi ya Uingereza resi ya farasi 2 tu-Manchester na Chelsea.

Huko Itali,mabingwa wa Itali Inter Milan wamepiga hatua nyengine karibu zaidi na kutwaa tena taji la Serie A walipoizaba jana Roma mabao 2:0 .Roma inanyatia taji kutoka nafasi ya pili.

Na huko Spian,Sevilla inayosimama nafasi ya pili ilizimwa sare 0:0 na Osasuna na hivyo ,imeiachia FC Barcelona uongozi wa pointi 2 kileleni mwa la Liga.

Nae stadi wa Barcelona, mbrazil Ronaldinho amempiku sas muingereza David Beckham kama “mchezaji anaelipwa fedha nyingi kabisa “ kuliko wote.Hii inatokana na orodha ya kila mwaka iliochapishwa katika jarida la FORBES mwishoni mwa wiki.

Ronaldinho alivuna dala milioni 31.3 mwaka jana wakati David Beckham aliondokea na dala milioni 30.9.Nafasi ya tatu katika orodha hii mpya anafuata Ronaldo.

Manchester United imesalia kileleni kuwa timu tajiri kabisa duniani ikifuatwa na Real Madrid ya Spain huku Arsenal ikinyatia nafasi ya tatu.Bayern Munich ya Ujerumani, imeangukia nafasi ya 4.

Wakati kesho kombe la klabu bingwa barani Ulaya-champions League-linarudi uwanjani kwa Bayern munich –mabingwa wa Ujerumani wakiumana na Ac Milan ya Itali,kombe la klabu bingwa barani Afrika nalo linarudi uwanjani mwishoni mwa wiki ijayo.Tayari ijumaa hii,Young Africans ya Tanzania,itateremka uwanjani kuumana na Esperence.

Katika kinyan’ganyiro cha kombe la Mataifa Afrika litakaloaniwa huko Ghana,mwakani, Ugandan cranes-timu ya taifa ya Uganda,haikuridhika na pigo ililopata la bao 1:0 kutoka Nigeria.Mpambano huo utarudiwa Cairo.

Tumalizie mkasa wa kifo kisichotazamiwa cha kocha wa Pakistan katika mashindano ya ubingwa wa dunia wa cricket Bob Woolmer, huko Caribbean:

Afrika Kusini inapanga kumfanyia marehemu ibada maalumu ya ukumbusho mjini Cape Town jumatano ijayo.Woolmer aliwahi kuwa kocha wa timu ya cricket ya afrika Kusini na ukoo wake ukiishi kwa miaka mingi mjini Cape Town.

Kocha huyo aliekua na umri wa miaka 58 alikutikana amezimia na baadae akafariki katika chumba chake hotelini,mjini Kingston,Jamaica.

 • Tarehe 02.04.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHcQ
 • Tarehe 02.04.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHcQ
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com