1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern mabingwa tena wa DFB Pokal

19 Mei 2014

Bayern Munich yatamba dhidi ya Borussia Dortmund na kuonesha kuwa wao ni mabingwa wa kweli Ujerumani , baada ya kunyakua taji la pili msimu huu la kombe la shirikisho DFB Pokal ,

https://p.dw.com/p/1C2am
DFB - Pokalfinale 2014 Borussia Dortmund gegen Bayern München
Bayern Munich mabingwa wa DFB PokalPicha: Reuters

Ligi katika bara la Ulaya zimefikia mwisho mwishoni mwa juma, wakati macho na masikio ya wapenzi wa michezo sasa yanageukia upande wa fainali za kombe la dunia.

Nchini Ujerumani lakini mwishoni mwa juma kulikuwa na mpambano wa kukata na shoka, wakati mafahali wawili katika soka la Ujerumani walipokutana katika uwanja wa Olimpiki mjini Berlin kuumana katika kuwania taji la kombe la shirikisho, kama linavyofahamika DFB Pokal.

Bayern Munich ambao wametawazwa kuwa mabingwa wa ligi ya Ujerumani Bundesliga kwa mara ya pili mfululizo, wameonesha ubabe wao tena baada ya kuwashanda mahasimu wao wakubwa Borussia Dortmund kwa mabao 2-0 katika mchezo uliohitaji timu hizo kucheza kwa dakika 120.

DFB - Pokalfinale 2014 Borussia Dortmund gegen Bayern München
Arjen Robben baada ya kupachika bao la kwanzaPicha: Reuters

Bayern Munich imethibitisha kuwa ni mshindi asiyeshindika katika soka la Ujerumani , baada ya mshambuliaji kutoka Uholanzi Arjen Robben kupachika bao la kuongoza na Thomas Muller akashindilia msumari wa mwisho katika jeneza la Borussia.

Goli mbalo halikuhesabiwa

Hata hivyo mchezo huo kama ulivyotarajiwa ulikuwa na matukio ya kukumbukwa, mojawapo ni goli la Borussia Dortmund ambalo lilionekana kuvuka mstari wa goli ambalo mwamuzi alishindwa kuliona. Mfungaji wa bao hilo alikuwa mlinzi wa Borussia Dortmund , Mats Hummels:

"Hii inakatisha tamaa. Goli hilo lilipaswa kuhesabiwa, na kama ingekuwa hivyo ingekuwa rahisi kwetu kushinda, kwasababu nafasi ingekuwa kubwa zaidi. Lakini pamoja na hayo haikuwa kitu kisichowezekana, kushinda mchezo huo. Lakini haiwezekani kutegemea tu tukio kama hilo. Ni sisi wenyewe ambao tumefanya hali kuwa hivi ilivyo."

Mlinzi wa kushoto wa Borussia Dortmund Marcel Schmelzer nae alikuwa na haya ya kusema kuhusiana na mchezo huo.

DFB - Pokalfinale 2014 Borussia Dortmund gegen Bayern München
Thomas Muller akishangiria bao la piliPicha: Reuters

"Muda wote tulikuwa sare, na wakati huo wote mchezo ulikuwa sawa, hadi wakati ambapo tulifunga bao letu, ambalo lilikataliwa. Baadaye kulikuwa na kutokuelewana kidogo upande wa ulinzi, ambapo tulipoteza mpira. Hadi wakati huo tulikuwa sawa kimchezo, na tulikuwa wa kwanza kupata bao."

Kwa upande wa washindi Bayern Munich hali haikuwa rahisi baada ya kutolewa katika ligi ya mabingwa Champions League dhidi ya Real Madrid wiki mbili zilizopita na kipigo cha mabao mengi nyumbani. Wadadisi wa soka walikuwa wakitafakari uwezo wa kimbinu wa kocha nyota Pep Guardiola. Mlinda mlango wa Bayern Munich Manuel Neuer amesema mchezo huo ulikuwa ni wa kujipima uwezo wao wa utulivu wa kichwa.

"Ni muhimu kila mara , kwani kwetu sisi lilikuwa ni suala la ukosoaji kuhusu utulivu wetu wa kichwa. Hilo tumelitimiza vizuri sana. Falsafa ambayo kocha wetu aliyotufahamisha kabla ya mchezo, ilitumika kikamilifu. Iwapo tungeshindwa kuitekeleza , leo tusingetoka na ushindi."

DFB - Pokalfinale 2014 Borussia Dortmund gegen Bayern München
Mats Hummels akishangiria bao ambalo halikuhesabiwaPicha: Reuters

Na mfungaji wa bao la kwanza kwa Bayern Munich Arjen Robben amekuwa mwiba kwa Dortmund kila mara hasa katika mchezo wa fainali. Robben alipachika bao la ushindi msimu uliopita katika fainali ya Champions League kule Wembley mwaka jana na mwishoni mwa wiki aliwaliza tena Dortmund kwa kupachika bao la kwanza.

"Itabaki kuwa fainali ya hali ya juu. Inabaki kuwa kombe la shirikisho , inabaki kuwa taji . Ndio sababu tulihitaji kushinda kwa hali yoyote ile. Watu wameona uwanjani , na sifa nyingi zikiendee kikosi kizima. Wengi walifikiri hatutaweza , nakini sasa tuko hapa tulipo, tumeweza kushinda. Tumefanikiwa tena kupata mataji mawili na tumekuwa na msimu mzuri kabisa."

Fußball Bundesliga 29. Spieltag Hamburger SV Bayer Leverkusen
Hamburg SV wakifurahia kubakia katika daraja la kwanza , BundesligaPicha: Stuart Franklin/Bongarts/Getty Images

Atletico Madrid waonja tamu

Kwingineko katika bara la Ulaya Atletico Madrid ilipata sare ya bao 1-1 dhidi ya Barcelona na point moja waliyoihitaji kunyakua taji lao la kwanza katika muda wa miaka 18. Real Madrid ambayo iliishinda Espanyol Barcelona kwa mabao 3-1 siku ya Jumamosi , imemaliza ikiwa ya tatu kwa kupata points 87, na hii ina maana Barca inashika nafasi ya pili katika ligi ya Uhispania La Liga.

Nchini Uingereza Arsenal ilipata kipindi cha kutisha katika mchezo wake wa fainali ya kombe la FA dhidi ya Hull City baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0 katika muda wa dakika nane za mchezo huo. Lakini Arsenal iliweza kurejea katika mchezo huo na kushinda kwa mabao 3-2 na kunyakua taji lake la kwanza katika muda wa miaka 9.

Hamburg bado ina hadhi ya daraja la juu

Nchini Italia Juventus Turin imekuwa timu ya kwanza nchini humo kuvuka points 100 katika ligi ya nchi hiyo Serie A baada ya kuishinda Cagliari kwa mabao 3-0 katika mchezo wao wa mwisho wa msimu huu siku ya Jumamosi.

Mabingwa wa zamani kombe la mabingwa wa Ulaya Hamburg SV wamerejea katika nafasi yao katika ligi ya daraja la kwanza nchini Ujerumani baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya timu ya daraja la pili ya SV Gruether Fuerth katika mchezo wao wa pili wa mchujo jana Jumapili.

Uganda yaangukia pua

Katika bara la Afrika Madagascar imebeza upangaji wa ubora wa timu duniani unaotolewa na shirikisho la kandanda duniani FIFA kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Uganda katika mchezo wa kufuzu kucheza katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika mwishoni mwa juma. Uganda , The Cranes wako nafasi 32 juu ya Madagascar katika bara la Afrika ikiwa ni pengo kubwa baina ya timu hizo.

Lakini walikuwa Madagascar ambao walikuwa wakitawala pambano hilo lililofanyika katika uwanja wa Mahajanga kaskazini mwa nchi hiyo na huenda wangeshinda kwa mabao mengi zaidi. Uganda hata hivyo itakumbana tena na Madagascar Mei 31 na The Cranes inabakia kuwa timu inayopigiwa upatu kusonga mbele.

Kenya ilitarajiwa kushinda kwa kiwango kikubwa dhidi ya visiwa vya Comoro, lakini walipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 katika uwanja wa Nyayo mjini Nairobi.

Tanzania ikaishinda Zimbabwe kwa bao 1-0 mjini Dar Es Salaam, Burundi ikatoka sare ya bila kufungana na Botswana , wakati Msumbiji ilishindilia Sudan kusini mabao 5-0 mjini Maputo.

Huko mjini Kigali nchini Rwanda jana(18.05.2014) kulifanyika mashindano ya kimataifa ya mbio ndefu , Marathon yanayojulikana kama Kigali Peace International Marathon ambapo Wakenya walitamba katika mbio hizo. Wanariadha zaidi ya elfu mbili kutoka sehemu mbali mbali duniani walishiriki katika mashindano hayo ikiwa ni awamu ya 10 tangu mashindano hayo yafanyike nchini Rwanda.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre /

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman