Bayern iko ngangari, Dortmund yateleza | Michezo | DW | 24.09.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Bayern iko ngangari, Dortmund yateleza

Baada ya mechi nne katika ligi ya soka ya Ujerumani - Bundesliga, Bayern Munich imekusanya pointi zote 12 na kufunga magoli 14, ikiwa ndio mwanzo wake mzuri zaidi kuwahi kushuhudiwa mwanzoni mwa msimu.

Fußball 1. Bundesliga 4. Spieltag Schalke 04 - Bayern München am 22.09.2012 in der Veltins-Arena in Gelsenkirchen Spieler von Bayern München bedanken sich bei den Fans Foto: Revierfoto

Fußball Bundesliga 4. Spieltag Schalke 04 - Bayern München

Jumanne, (25.09.2012) Bayern itakuwa nyumbani kwa Wolfsburg, timu ambayo imeshindwa mechi 16 kati ya 17 zilizochezwa mjini Munich, huku sare ya pekee ikiwa mnamo mwaka wa 2001.

Kiungo Mholanzi Arjen Robben aliwaambia waandishi habari baada ya Bayern kuwalaza Schalke magoli mawili kwa sifuri siku ya Jumamosi kuwa timu yake iko katika hali nzuri sasa.

Msimu uliopita, Bayern ilionekana kuwa moto wa kuotea mbali lakini mwishoni mwa msimu ikazembea na kushindwa kunyanua hata kombe moja baada ya kumaliza ya pili katika ligi ya Bundesliga, na kushindwa na Chelsea katika fainali ya kombe la Mabingwa barani Ulaya na vile vile kombe la shirikisho.

Wachezaji wa Dortmund walisalia kujishika vichwa baada ya kichapo

Wachezaji wa Dortmund walisalia kujishika vichwa baada ya kichapo

Katika ushindi wa magoli mawili kwa sifuri siku ya Jumamosi dhidi ya Schalke, kocha Jupp Heynckes alifanya mabadiliko matatu katika kikosi kilichoipiku Valencia katika mchuano wa Ligi ya Mabingwa katikati ya wiki na huenda akatumia kikosi hicho hicho katika mchuano dhidi ya Wolfsburg.

Cha kushangaza ni kuwa Bayern wanaongoza ligi ya Bundesliga, kwa pamoja na Eintracht Frankfurt, ambao Ijumaa waliandikisha rekodi mpya ya Bundesliga kwa kuwa klabu ya kwanza kupandishwa daraja na kushinda mechi nne mfululizo za ufunguzi wa msimu.

Sasa watacheza nyumbani dhidi ya mabingwa watetezi Borusia Dortmund ambao rekodi yao ya mechi 31 bila kushindwa katika Bundesliga ilifikishwa kikomo Jumamosi baada ya kupigwa magoli matatu kwa mawili na SV Hamburg. Beki wa Dortmund. Mechi nyingine za kesho Jumanne Greuther Fuerth itakuwa mwenyeji wa Fortuna Duesseldorf huku Schalke 04 wakiwa nyumbani dhidi ya Freiburg.

Jumatano, nambari tatu wa ligi Hanover ambao waliduwazwa magoli matatu kwa moja na Hoffenheim jana Jumapili, watakuwa nyumbani kwa Nuremberg ambao pia wamekuwa na matokeo bora mwanzoni mwa msimu na wako katika nafasi ya sita. Timu zote zina pointi saba baada ya kucheza mechi nne.

Pia Jumatano, Borussia Moenchengladbach, waliotoka sare ya kufungaan goli moja kwa moja na Bayer Leverkusen siku ya Jumapili, watakuwa nyumbani kwa Hamburg, huku VfB Stuttgart, waliopata pointi yao ya pili msimu huu, baada ya kutoka nyuma magoli mawili na kulazimisha sare ya magoli mawili kwa mawili nyumbani kwa Werder Bremen wakipambana na Hoffenheim. Mechi za mwisho zitakuwa kati ya Augsburg na Leverkusen, na Freiburg dhidi ya Werder Bremen.

John Terry astaafu soka ya kimataifa

John Terry ameamua kuzitundika njumu katika soka ya kimataifa

John Terry ameamua kuzitundika njumu katika soka ya kimataifa

Beki wa timu ya taifa ya soka ya Uingereza John Terry ametangaza kustaafu kwake kutoka soka ya Kimataifa muda mfupi kabla ya Shirikisho la Soka Uingereza FA kuanza uchunguzi kuhusu madai kuwa alimtolea matamshi ya kibaguzi mchezaji mwenzake.

Beki huyo wa klabu ya Chelsea aliichezea timu ya taifa ya Uingereza mechi 78. mahakama moja ya London ilimpata Terry bila hatia ya kutoa matashi ya kibaguzi kutokana madai kuwa alimtusi beki wa timu ya QPR Anton Ferdinand wakati wa mchuano mnamo mwaka wa 2011. Shirikisho la FA lilimpokonya Terry unahodha wa timu ya taifa mnano mwezi Februari na jambo lililomfanya kocha wa timu Fabio Capello kujiuzulu wadhifa wake.

Terry amesema sasa anaangazia kuchezea klabu yake ya Chelsea na kuendelea kushindania mataji ya nyumbani na Ulaya. Akizungumzia uamuzi huo, mkufunzi wa timu ya taifa ya Uingereza Roy Hodgson amesema ameikubali hatua hiyo ijapokuwa anasikitika kuwa Terry aliamua kufanya hivyo.

Tukisalia huko Uingereza, ni kwamba mkwaju wa penalti katika dakika za mwisho mwisho wake Robin van Persie uliipa Manchester United ushindi wa magoli mawili kwa moja nyumbani kwa Liverpool jana Jumapili katika mchuano wa uhasimu wa Kaskazini Magharibi ambao ulikuwa wa kwanza uwanjani Anfield tangu kuchapishwa ripoti ya mkasa wa Hillsborough. Chelsea wako kileleni na tofauti ya pointi moja baada ya kuwafunga Stoke City goli moja kwa sifuri siku ya Jumamosi. Mabingwa watetezi Manchester City walikabwa sare ya goli moja kwa moja na Arsenal, Laurent Koscielny akifunga bao la kusawazisha katika dakika za mwisho mwisho baada ya Joleon Lescott kuwaweka City kifua mbele uwanjani Etihad.

Bondia Corri auawa na majambazi

Na katika habari za tanzia, bingwa wa zamani wa ndondi katika uzani wa wa juu MuaAfrika Kusini Cornelius Sanders kwa jina la utani Corri ameuawa jana kwa kupigwa risasi na majambazi waliovamia sherehe ya kuadhimisha miaka 21 ya kuzaliwa kwa mpwa wake.

Sanders mwenye umri wa miaka 46 alipigwa risasi mkononi na tumboni wakati majambazi walipovamia mgahawa mmoja nje ya mji wa Brits katika mkoa wa Kaskazini Magharibi ambako yeye pamoja na jamaa wengine wa familia yake walikuwa wakihudhuria sherehe ya siku ya kuzaliwa kwa mpwa wake.

Alikimbizwa hospitalini lakini akafariki kutokana na majeraha aliyopata. Sanders alishinda taji la Shirikisho la Ndondi Ulimwenguni WBO mnamo mwaka wa 2003 uzani wa juu baada ya kumrambisha sakafuni kwa nokout bondia wa Ukraine Wladmir Klitschko. Kati ya mapigano 46 katika taaluma yake, alishindwa manne pekee.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/DPA/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu