Bashir asema hana kinyongo na Sudan ya kusini kujitenga. | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.12.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Bashir asema hana kinyongo na Sudan ya kusini kujitenga.

Wakati kura ya maoni itakayoamua mustakabali wa kugawika Sudan ikikaribia kufanyika, Rais wa Sudan, Omar al Bashir, ameahidi kusaidia kuwepo kwa udhabiti, usalama na udugu katika taifa hilo linalotarajiwa la Kusini.

Rais wa Sudan Omar al Bashir (kulia) akiwa na Rais wa serikali ya Sudan ya kusini, Salva Kiir Mayardit (kulia).

Rais wa Sudan Omar al Bashir (kulia) akiwa na Rais wa serikali ya Sudan ya kusini, Salva Kiir Mayardit (kulia).

Rais wa Sudan, Omar Hassan al Bashir, amesema hawataukataa uamuzi wa ndugu zao wa Sudan ya kusini wa kujitenga na kuanzisha taifa lao, na kwamba watawasaidia kulijenga taifa lao kwa sababu wanataka taifa lililo salama na imara kutokana na kwamba iwapo nchi hiyo mpya huru itakabiliwa na matatizo, hali hiyo pia itawakumba na wao.

Rais Bashir ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na maelfu ya wafuasi wake katika jimbo la Gezira, hotuba ambayo ilirushwa moja kwa moja na televisheni ya nchi hiyo.

Rais huyo wa Sudan alisema kuwa atakuwa wa kwanza kulitambua taifa hilo la Sudan ya kusini iwapo itaaamua kujitenga katika kura ya maoni itakayofanyika kwa njia ilio huru na ya haki katika wiki zisizozidi mbili kuanzia sasa.

Aidha amesema ataupokea pia uamuzi wa kutojitenga kwa pande hizo mbili.

Zaidi ya Wasudan kusini milioni 3.5 wamejiandikisha kuweza kushiriki zoezi la upigaji kura hiyo ya maoni, ambayo itawapa nafasi kupiga kura kama wanataka kubakia katika umoja na upande wa kaskazini ama kujitenga nao.

Kura hiyo ya maoni inatokana na makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2005, yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa takriban miaka 22 na kusababisha vifo vya karibu wa tu milioni mbili na kuwaacha wengine kadhaa bila ya makaazi.

Katika hatua nyingine, Katibu mkuu wa Umoja wa nchi za kiarabu, Amr Moussa, amesema haoni dalili zozote za Sudan ya kusini na ya kaskazini kurudi tena vitani, katika kipindi hiki cha kuelekea kura ya maoni itakayoigawa nchi hiyo.

Akizungumza na Waandishi wa habari mjini Khartoum, wakati wa ziara yake ya siku mbili, itakayompeleka pia katika mji mkuu wa Sudan ya kusini, Juba, Bwana Amr Mussa amesema kinachoendelea kati ya pande hizi mbili ni tofauti kabisa na uwezekano wa kutokea mapigano na kwamba kuna nia njema ya kisiasa.

Aidha amesema kwamba atatuma kikundi cha waangalizi katika zoezi hilo la upigaji kura la Januari 9.

Katika ziara yake hiyo pia atajadili masuala mbalimbali baada ya kura hiyo ya maoni na pia jinsi ya kuimarisha uhusiano kati ya pande hizo mbili katika siku za baadaye.

Baadhi ya watu wamekuwa na wasiwasi kwamba kujitenga kwa Sudan ya Kusini na masuala kadhaa ambayo mpaka sasa hayajapatiwa ufumbuzi yanaweza yakasababisha pande hizo mbili kutumbukia tena vitani.

Tangu mwezi Julai mwaka huu Sudan ya kusini na Kaskazini hazijafanikiwa katika mazungumzo yao kujadili masuala muhimu, ikiwemo maandalizi ya uraia baada ya pande hizo kujitenga na ugawanaji wa rasilimali kama vile mafuta na masuala ya ulinzi.

Mwandishi: Halima Nyanza(ap, afp)

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 29.12.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/zr2S
 • Tarehe 29.12.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/zr2S