Barroso achaguliwa tena. | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.09.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Barroso achaguliwa tena.

Jose Manuel Barroso amechaguliwa tena kuwa rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya.

default

Jose Manuel Barroso , amechaguliwa tena kuwa rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya.

Bunge la Ulaya leo limemchagua tena bwana Jose Manuel Barroso kutumikia kipindi kingine cha miaka mitano katika wadhifa wa rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya.

Barroso alipata kura 382 na kura 219 zilipigwa kumpinga. Wabunge 117 waliamua kutopiga kura. Kuchaguliwa kwa Barroso leo kunamaliza utatanishi uliochukua miezi kadhaa miongoni mwa wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Barroso ameahidi kushirikiana na bunge kwa undani zaidi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.Barroso amesema anadhamiria kuimarisha demokrasia katika Umoja wa Ulaya.

Spika wa bunge la Ulaya Jerzy Buzek amempongeza bwana Barroso kwa kuchaguliwa tena na ameeleza matumaini juu ya kushirikiana naye katika kukabiliana na alichoita changamoto nyingi. Spika huyo bwana Buzek amesema bunge la Umoja wa Ulaya litakuwa na kazi nyingi na kwamba anatumai bwana Barroso atashirikiana na wote katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Waziri Mkuu wa Sweden Fredrik Reinfeldt ambae kwa sasa unaoungoza Umoja wa Ulaya amesema kuchaguliwa tena kwa bwana Barroso ni habari nzuri.

Kuchaguliwa tena kwa bwana Barroso kulitarajiwa kutokana na yeye kuwa mjumbe wa pekee.Watu wanaomuunga mkono wamesema kuteuliwa kwake tena kunawakilisha uendelevu na uthabiti barani Ulaya.Lakini wanaompinga wanasema mtazamo wake juu ya mgogoro wa uchumi ulikuwa dhaifu.

Mbunge wa chama cha social demokratik Martin Shulz amehoji kwamba hajawahi kutokea rais dhaifu wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya kama Barroso.

Licha ya ushindi wake katika uchaguzi Barroso alipata kura chache kulinganisha na mara ya kwanza alipoingia katika wadhifa huo mnamo mwaka 2004.

Wakati huo Barroso alipata kura 413. Hatahivyo alikuwa tayari anaungwa mkono kwa kauli moja na viongozi wa nchi zote 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Mwandishi/Mtullya Abdu/AFPE

Mhariri/Othman Miraj

 • Tarehe 16.09.2009
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/JiGL
 • Tarehe 16.09.2009
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/JiGL

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com