1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barcelona: Wanne wafikishwa mahakamani

Lilian Mtono
22 Agosti 2017

Watuhumiwa wanne waliosalia ambao ni wanachama wa kundi la kigaidi lililohusika na mashambulizi pacha nchini Uhispania wamefikishwa mahakamani ambako watashitakiwa, ikiwa ni baada ya wengine wanane kuuawa.

https://p.dw.com/p/2icml
Spanien Ripoll Verhaftung Verdächtige Polizei
Picha: picture-alliance/AP Photo/F. Seco

Watuhumiwa hao walisindikizwa chini ya ulinzi mkali kuelekea mahakama ya Kitaifa, inayohusika na kesi za ugaidi, ambako jaji ataamua kuhusu iwapo watuhumiwa hao wana kesi ya kujibu kuhusiana na mashambulizi hayo pacha yalihusisha kuwakanyaga watembea kwa miguu kwa lori na kusababisha vifo vya watu 15 na wengine 120 kujeruhiwa.

Vyombo vya habari vya Uhispania vinawataja watuhumiwa hao kuwa ni Driss Oukabir, Mohammed Aalla, Sahl el Karib na Mohamed Houli Chemal, na wanafikishwa mahakamani leo mjini Madrid.

Mnamo, hapo jana Jumatatu polisi ya Uhispania ilifanikiwa kumuua mtuhumiwa aliyekuwa anasakwa Younes Abouyaaqoub anayehusishwa na shambulizi la kigaidi mjini Barcelona, na kukamilisha msako mpana wa mtu huyo raia wa Morocco aliyekuwa amevaa mkanda wa vilipuzi bandia na kupiga kelele "Allah Akbar", akimaanisha Mungu ni Mkubwa alipokuwa akifanya mauaji hayo.

Yacoub alikuwa ni mwanachama pekee aliyesalia kati ya 12 wa kundi hilo la kigaidi linalotuhumiwa kuandaa mashambulizi wiki iliyopita katika mji ya Barcelona na mji wa Pwani wa Cambrils, ambayo kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu lilidai kuyafanya.

Jana jumatatu, Rais wa Marekani Donald Trump alipokuwa akizungumzia mikakati ya Marekani kuelekea vita vya nchini Afghanistan, amezungumzia pia mashambulizi hayo ya Hispania kwa kutaka mkakati wa kupambana na makundi ya itikadi kali, huku akiwatuhumu vikali kwa kufanya mauaji kwa watu wasio na hatia.

Spanien | Pressekonferenz der katalischen Behörden zum Anschlag in Barcelona | Polizeichef Trapero, Innenminister Forn und Justizminister Mundo
Mkuu wa polisi wa mkoa wa Catalan Joseph Lluis Trapero akithibitisha kuuawa kwa washambuliaji haoPicha: Getty Images/AFP/L. gene

Watu wanne walitiwa kizuizini na waliosalia waliuawa ama na polisi au katika mripuko uliodhaniwa kuwa watuhumiwa wenyewe waliripua kwa bahati mbaya katika nyumba waliyokuwa wakitengeneza mabomu, katika mji wa ufuoni, Alcanar. Mkuu wa polisi wa jimbo la Catalonia, Joseph Lluis Trapero alithibitisha hapo jana kuwa miongoni mwa waliouawa ni Imamu raia wa Morocco ambaye alikuwa mtu muhimu kwenye kundi hilo Abdelbaki Es Satty.

Polisi imesema Imamu huyo alikuwa kizuizini kwa muda na kuna wakati alikuwa na mawasiliano na mtuhumiwa aliyekuwa akisakwa kwa mashitaka ya ugaidi, lakini hakuwahi kushitakiwa kwa matukio yoyote yanayohusiana na ugaidi.

Nchini Morocco, katika mji wa M'rirt, jamaa ya Abouyaaqoub wamemtuhumu Imamu huyo kwa kuwapa mafunzo ya itikadi kali kijana huyo mdogo, pamoja na kaka yake Houssen.

Wachunguzi wanataka kulichunguza na kulielezea kundi hilo lenye makazi yake katika mji mdogo ulioko mpakani wa Ripoll chini ya milima ya Pyrenees, Kaskazinimashariki mwa Uhispania.

Kuripuka kwa mabomu katika nyumba mjini Alcanar, kunadhaniwa kuwa kuliwafanya washambuliaji hao kuandaa mpango mwingine, na ndipo badala yake walitumia malori kuingia kwenye maeneo yenye watu wengi ya Las Ramblas mjini Barcelona na kuua watu 13, na kujeruhi zaidi ya 100. Masaa kadhaa baadae, shambulizi kama hilo lilifanywa mjini Cambrils na kuua mwanamke mmoja.

Mamia ya waumini wa Kiislamu wameandamana jana katika eneo la Las Ramblas, wakiwa na mabango yenye ujumbe "Tunapinga ugaidi" na "Sisi ni waislamu, sio magaidi".

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/EAP

Mhariri: Josephat Charo