Baraza la Wawakilishi lapitisha mswada kuhusu vita vya Iraq. | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 26.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Baraza la Wawakilishi lapitisha mswada kuhusu vita vya Iraq.

Baraza la Wawakilishi nchini Marekani limeidhinisha mswada unaopendekeza kuwekwa muda maalum wa kuyaondoa majeshi ya Marekani nchini Iraq. Wabunge hawakuutilia maanani vitisho vya Rais George W. Bush kuuangusha mswada huo unaoshughulikia fedha za kugharamia vita vya Iraq. Mkuu wa majeshi ya Marekani nchini Iraq, Jemedari David Patraeus, alikuwepo bungeni kuwarai wabunge hao kuregeza msimamo wao lakini akaambulia patupu.

Spika wa Bunge la Marekani, Bi Nancy Pelosi. Bi Pelosi amekiongoza chama chake cha Demokratic kupitisha mswada wa vita bungeni.

Spika wa Bunge la Marekani, Bi Nancy Pelosi. Bi Pelosi amekiongoza chama chake cha Demokratic kupitisha mswada wa vita bungeni.

Mswada huo uliopitishwa kwa kura 218 dhidi ya kura 208, unaruhusu kutolewa kiasi dola bilioni 124 kwa shughuli za kijeshi nchini Iraq na Afghanistan lakini kwa masharti kwamba majeshi ya Marekani yaanze kuondoka katika nchi hizo mbili kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu.

Mswada huo unatarajiwa pia kupigiwa kura na kuidhinishwa na baraza la Senate, kabla ya kuwasilishwa kwa Rais George W. Bush ambaye amekuwa akisisitiza kwamba ataupinga kwa vyovyote vile.

Msemaji wa Rais Bush, Bi Dana Perino, amesema hatua hiyo ya wabunge wa chama cha Demokratic itasababisha harakati hizo za kivita kuchukua muda mrefu.

Msemaji huyo amesema Rais George Bush anataka baraza la Senate liuidhinishe mswada huo haraka iwezekanavyo ili naye atumie mamlaka yake kuuangusha.

Bi Dana Perino amesema itawabidi wabunge baadaye kushirikiana na Rais George Bush kutayarisha mswada utakaozingatia nasaha ya wakuu wa kijeshi na pia utakaohakikisha usalama wa Wamarekani.

Spika wa Bunge la Marekani, ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Democratic bungeni, Bi Nancy Pelosi, alizungumza kuhusu maelfu ya Wamarekani walioathiriwa na vita na pia Wairaq maelfu waliouawa kutokana na vita hivyo.

Bi Nancy Pelosi alilalamikia gharama ambayo Marekani imeingia kwa sababu ya kujihusisha na vita nchini Iraq.

O TON NANCY PELOSI

"Tumeyahusisha majeshi yetu katika shughuli nyingi za kijeshi zisizofaa, vita hivi vimekuwa kikwazo kikubwa kwenye harakati za kuwalinda raia Wamarekani. Wamarekani hawajawa salama kutokana na vita nchini Iraq, badala yake vita hivyo vimeuvuruga uwezo wa kulilinda taifa letu dhidi ulimwenguni"

Spika huyo wa bunge la Marekani amesema wanajeshi pamoja na jamaa zao wamejitolea vya kutosha wala haifai kwa Rais George W. Bush kutaka idhini ya kuendeleza vita visivyokuwa na mwisho.

Bi Nancy Pelosi amemtolea wito Rais George W. Bush kuuidhinisha mswada huo ili kutoa fursa ya kushughulikia vilivyo vita dhidi ya ugaidi ambavyo ndivyo tishio kubwa kwa maisha ya Wamarekani.

Wabunge wa Democratic wamepiga kura hiyo ya kuidhinisha kutoa muda maalumu wa kuyaondoa majeshi ya Marekani Iraq wakati ambapo kura ya maoni ya hivi karibuni inaonyesha Wamarekani wengi wanaunga mkono kuondolewa majeshi nchini Iraq wakiamini kwamba ushindi hautapatikana kamwe.

Kwa mujibu wa matokeo ya kura ya maoni ya shirika la habari la NBC na Gazeti la Wall Street, asilimia 56 ya Wamarekani wanataka kupangwa muda maalumu wa kuyaondoa majeshi nchini Iraq ilhali asilimia 37 sawa na Rais wao, George Bush, wanapinga uamuzi huo.

Hata hivyo mswada huo unapendekeza kiasi zaidi cha fedha kuliko kiasi ambacho utawala wa Marekani ulikuwa umependekeza kugharamia shughuli za kijeshi nchini Iraq na Afghanistan.

Pia wabunge hao wamesema majeshi ya Marekani yanapaswa kuanza kuondoka nchini Iraq mwezi Oktoba mwaka huu na ikiwezekana majeshi yote yawe yameshaondoka kufikia mwisho wa mwezi Machi mwakani.

 • Tarehe 26.04.2007
 • Mwandishi Omar Babu
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB4R
 • Tarehe 26.04.2007
 • Mwandishi Omar Babu
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CB4R

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com