1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama lapitisha azimio juu ya Kongo

31 Januari 2014

Kwa kauli moja Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambalo linapiga marufuku silaha na uungaji mkono wa nchi jirani kwa makundi ya waasi nchini Kongo.

https://p.dw.com/p/1Azwd
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, New York.
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, New York.Picha: Reuters

Azimio hilo Namba 2136 limezitaka nchi za Maziwa Makuu kutokuyaunga mkono kwa aina yeyote ile makundi ya wapiganaji mashariki mwa Kongo, ingawa si Rwanda wala Uganda zilizotajwa kwa majina, licha ya kuwa katika ripoti kadhaa za Umoja huo, nchi hizo zimekuwa zikinyooshewa kidole cha tuhuma.

Vile vile, Baraza la Usalama limezihimiza serikali za nchi za Maziwa Makuu kulishuhulikia ipasavyo swala la waasi wa M23 ili wasije tena kuchukuwa silaha.

Vikwazo vya Umoja wa Mataifa vitawekwa sio tu kwa wababe wa kivita, bali pia kwa watu wanaohusika na ujangili pamoja na biashara ya pembe za ndovu.

Pia Baraza hilo la Usalama limeunga mkono Kamati yake ya Wataalamu kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ingawa serikali ya Rwanda imewatupia lawama wataalamu hao.

Kwa azimio hili, sasa marufuku ya silaha kwa Kongo imeongezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja, sambamba na muhula wa Kamati ya Wataalamu wa Umoja wa Mataifa kwa Kongo, ambayo pia imepewa mwaka mmoja zaidi.

Vita vya maneno viliibuka kwenye chumba cha mikutano cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baina ya mabalozi wa Rwanda na Kongo kwenye Umoja huo.

Vita vya maneno vya Rwanda na Kongo

Mara tu baada ya kuidhinishwa kwa azimio hilo, Balozi wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa, Eugene-Richard Gasana, alipewa nafasi ya kuelezea maoni yake kuhusu ripoti ya mwaka ya Umoja wa Mataifa, ambayo inaituhumu nchi hiyo kuendelea kuliunga mkono lililokuwa kundi la waasi la M23, ambapo Balozi alisema kwamba alipiga kura ya ndio kwa shingo upande.

Rais Paul Kagame wa Rwanda (kushoto) katika moja ya mikutano aliyokutana na Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (kulia).
Rais Paul Kagame wa Rwanda (kushoto) katika moja ya mikutano aliyokutana na Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (kulia).Picha: picture-alliance/dpa

"Tulipitisha Azimio hilo siyo kwa hiyari yetu. Ripoti hiyo imepotoshwa na hatuikubali hata kidogo. Lakini tujipe matumaini huenda mwaka ujao wataalamu hao wataandaa kitu cha muhimu ambacho kitasaidia raia wa Kongo kujikwamua kutoka kwenye matatizo waliyonayo." Alisema Balozi Gasana.

Lakini Balozi wa Kongo kwenye Umoja wa Mataifa, Ignace Gata, alikwenda umbali wa kuituhumu moja kwa moja Rwanda kuhusika na machafuko ya Kongo kwa kipindi kirefu, akiutolea wito Umoja wa Mataifa kukomesha kile alichokiita "kiburi cha Rwanda."

"Sisi tumeionyesha jamii ya kimataifa kwamba mauwaji ya kimbari ni tukio lililotokea Rwanda na yalifanyika kwenye ardhi ya Rwanda na baina ya Wanyarwanda, na Kongo haikuhusika kwa karibu au kwa umbali na mauwaji hayo ya halaiki. Tulitaka kujibu matamshi ya Balozi wa Rwanda ambae ameonyesha kiburi cha nchi yake katika kukiuka mikataba ya kimataifa."

Vita hivyo vya maneno viliendelea kwa sababu kila upande ulilazimisha kujibu papo hapo tuhuma za upande mwengine, hali iliyomlazimisha Mwenyekiti wa Baraza la Usalama, Balozi Mohammed Al-Allaf wa Jordan, kuukomesha mjadala huo.

Mwandishi: Saleh Mwanamilongo/DW NewYork
Mhariri: Mohammed Khelef