Baraza la Usalama lajadili shambulio la Beit Hanoun | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.11.2006
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Baraza la Usalama lajadili shambulio la Beit Hanoun

Israel katika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York, ilishambuliwa vikali kuhusu mashambulio yake yalioua raia 18 katika Ukanda wa Gaza.

Nchi za Kiarabu ziliongoza mito ya kulaani vikali mashambulio yaliofanywa na Israel siku ya Jumatano katika mji wa Beit Hanoun kwenye Ukanda wa Gaza na kusababisha vifo vya raia 18 wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan ameeleza huzuni na wasi wasi wake juu ya hasara ya maisha ya raia.

Hata Ban Ki-Moon atakaempokea Kofi Annan kama katibu mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasi wasi wake kuhusu shambulio hilo la Israel. Ametoa mwito wa kufanywa mkutano kati ya Kofi Annan na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili njia za kuzuia mgogoro huo kushika kasi katika maeneo yaliokaliwa.

Kwa upande mwingine nchi za Kiarabu zimelitaka Baraza la Usalama lipitishe azimio kutoa mwito wa kukomesha moja kwa moja mashambulio katika eneo la Gaza.Vile vile tume ya Umoja wa Mataifa isimamie makubaliano ya kuacha mapigano kama ilivyofanywa kusini mwa Lebanon,baada ya vita vya siku 34 kati ya Israel na Hezbollah kumalizika mwezi wa Agosti.

Mjumbe wa Wapalestina katika Umoja wa Mataifa,Ryad Mansour amesema shambulio lililofanywa na Israel ni ugaidi wa kitaifa;ni vita vya uhalifu na wale waliohusika lazima wawajibike kuambatana na sheria ya kimataifa. Uvunjaji wa sheria na kutoadhibiwa kwa Israel lazima ukomeshwe;na Wapalestina wapewe haki zao ikiwa ni pamoja na haki yao ya kulindwa kama umma wa kiraia uliokaliwa.

Lakini mwanadiplomasia wa Israeli amesisitiza kuwa shambulio la siku ya Jumatano katika mji wa Beit Hanoun lilifanywa kwa kosa.Amesema,Israel inasikitishwa na tukio hilo na inajitahidi iwezavyo kuzuia jambo kama hilo kutokea mara nyingine.Akiendelea,mjumbe huyo wa Israel alisema,ikiwa ugaidi wa Wapalestina hautoendelea na makombora ya Qassam yatasita kurushwa Israel kutoka eneo la Gaza,tukio la Beit Hanoun lisingetokea.

Na ripoti za hii leo zinasema makundi ya Hamas na Fatah yamekubali kutowaingiza wanasiasa mashuhuri katika serikali mpya ya umoja,inayojadiliwa kuundwa.Makundi hayo mawili yanayohasimiana yamekuwa yakijaribu kuunda serikali wanaosema itakuwa serikali ya umoja ya wataalamu.

Inatumainiwa kuwa serikali mpya huenda ikazishawishi nchi za magharibi kuregeza vikwazo vilivyowekwa baada ya chama cha Hamas kushika madaraka mwezi wa Machi.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com