Baraza la Seneti Marekani lamwondolea hatia Trump | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.02.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Trump aibuka kidedea katika mashtaka yaliyomkabili

Baraza la Seneti Marekani lamwondolea hatia Trump

Baraza la seneti mjini Washington limemtakasa rais Donald Trump, katika kesi ambamo alikuwa akishutumiwa na wabunge wa chama cha Democratic kutumia vibaya madaraka yake na kutatiza kazi za Baraza la Wawakilishi.

Katika kura ambazo, isipokuwa moja tu, zimefuata msingi wa vyama, maseneta 52 wamemwondolea hatia Trump, dhidi ya 48 waliotaka afukuzwe kazi. Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu ya Marekani John Roberts ndiye aliyeyatangaza matokeo hayo.

''Katika shauri hili la mashtaka, maseneta 48 wamesema Donald John Trump anayo hatia kwa makosa aliyoshtakiwa, maseneta 52 wamesema hana hatia kwa mashtaka hayo. Waliomkuta na hatia hawafiki theluthi mbili ya maseneta waliopo. Kwa hiyo Rais Donald John Trump hakukutwa na hatia katika shauri hili la mashtaka.'' Amesema Jaji Roberts.

USA Präsident Donald Trump (Imago Images/Zumapress/B. Cahn)

Rais wa Marekani Donald Trump, kitisho dhidi ya utawala wake kimeondolewa

Rais Donald Trump alikuwa akikabiliwa na shutuma za kutumia vibaya madaraka yake, kwa kumshinikiza rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kumchunguza makamu wa zamani wa Rais Joe Biden, ambaye anaweza kuwa mpinzani wa Trump katika uchaguzi wa rais wa mwezi Novemba mwaka huu.

Mitt Romney aiasi kambi yake 

Warepublican wanaolithibiti baraza la seneti wamepiga kura 52 kumtakasa Trump, huku mmoja tu, Mitt Romney akijiunga na Wademocrat na kufikisha idadi ya kura 48 zilizotaka Trump atimliwe kutoka madarakani.

Shitaka la pili dhidi ya Trump lilikuwa kulitatiza baraza la wawakilishi kutekeleza majukumu yake kwa kuwazuia maafisa wa utawala wake kutoa ushahidi mbele ya baraza hilo. Kuhusu shitaka hili, Romney amejiunga na Warepublican wenzake na kuwashinda Wademocrat kwa kura 53 dhidi ya 47.

Utakasaji usio na thamani

Akizungumza kufuatia matokeo hayo, kiongozi wa maseneta Wademocrat walio wachache, Chuck Schumer, amesema kura iliyomuondoa hatiani Trump haina thamani yoyote, kwa sababu Warepublican walikataa kata kata kusikiliza mashahidi. Schumer amesema anatumai Wamarekani watajua kilichotokea.

USA Washinton | Auftakt des Amtenthebungsverfahrens gegen Trump: Chuck Schumer (picture-alliance/abaca/S. Reynolds)

Kiongozi wa walio wachache katika Baraza la Seneti la Marekani, Chuck Schumer

''Naamini Wamarekani watajua kuwa kilichotokea ni kisa cha kufunika makosa kikubwa zaidi katika historia ya nchi yetu. Naamini kwamba Wamarekani watajua upande gani umesimamia ukweli, na upi uliogopa ukweli na kuufichaficha. Lakini, hatua kwa hatua, ushahidi zaidi utaibuka, na Walipublican watawajibishwa kwa namna walivyopiga kura.'' Amesema Seneta Schumer.

Kiongozi mwingine wa chama cha Democratic, spika wa baraza la wawakili Nancy Pelosi, amewashutumu Warepublican kufanya alichokiita ''kuhalalisha uvunjifu wa sheria, na kuupa kisogo mfumo wa wizani wa mamlaka ya mihimili ya utawala''.

Wachambuzi wa kisiasa wanasema Trump, ambaye ni rais wa tatu kufunguliwa mashitaka nchini Marekani, na wa kwanza kugombea muhula wa pili baada ya mchakato huo dhidi yake, atayatumia matokeo ya kumtakasa kama turufu katika kampeni ya kuwania muhula wa pili.

ape, afp

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com