Baraza la Seneti kusikiliza shauri dhidi ya Trump | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.01.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Baraza la Seneti kusikiliza shauri dhidi ya Trump

Vifungu vya mashtaka yanayomkabili rais Donald Trump vitasomwa leo mbele ya Baraza la Seneti mjini Washington hatua inayofungua rasmi shauri la kihistoria linalotishia kumuondoa madarakani kiongozi huyo wa Marekani.

Kiongozi wa chama cha Republican katika Baraza la Seneti Mitch McConnell amesema vifungu vya mashtaka vitasomwa baadae leo jioni  baada ya baraza hilo kuvipokea rasmi kutoka Baraza la Wawakilishi la Bunge la Marekani.

Wabunge saba wa Democrats wakiongozwa na mbunge Adam Schiff ndiyo wameteuliwa kuendesha mashtaka dhidi ya Trump yanayojumuisha matumizi mabaya ya madaraka na kujaribu kuzuia upatikanaji haki.

Shauri dhidi ya kiongozi huyo litafunguliwa rasmi Januari 21 ambapo Jaji wa mahakama ya juu nchini Marekani  John Roberts ataapishwa kuwa mwenyekiti na maseneta watakula kiapo cha kuwa wajumbe wa baraza la kutoa hukumu kwenye shauri hilo.

Hatua ya mchakato huo kupelekwa mbele ya Baraza la Seneti inafuatia kura ya Baraza la Wawakilishi ya Disemba 18 iliyoidhinisha mchakato wa kumshtaki Trump kwa kupitisha vifungu vya mashtaka.

Shauri dhidi ya trump limechelewa 

USA Senat bestätigt umstrittenen Richterkandidaten Kavanaugh | Mitch McConnell (Reuters/J. Ernst)

Kiongozi wa Republican kwenye Seneti, Mitch McConnell

Hata hivyo shauri mbele ya Seneti limechelewa kidogo baada ya spika wa bunge Nancy Pelosi kuzuia kwa muda kuwasilisha vifungu vya mashtaka ili kumshinikiza kiongozi wa wa walio wengi katika Seneti McConnell kutoa amri kwa mashahidi na nyaraka zilizozuiliwa na ikulu ya White House kuwasilishwa wakati wa kesi hiyo.

McConnell amepuuza wito huo akisema suala hilo litaamuliwa wakati shauri litakapofunguliwa na zaidi litategemea hoja zitakazowasilishwa mezani katika mchakato utakauchukua karibu wiki mbili.

Trump anatuhumiwa kuzuia kwa siri msaada wa dola za Marekani milioni 391 kwa Ukraine kati ya Julai na Septemba iliyopita ili kuishinikiza serikali mjini Kiev kufungua uchunguzi dhidi ya makamu wa rais wa zamani wa Marekani Joe Biden.

Biden anazingatiwa kuwa hasimu wa kisiasa wa rais Trump kwa sababu anapewa nafasi muhiu ya kuteuliwa kuwa mgombea wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa rais wa mwaka huu.

Wademocrats wachochea moto

Siku ya Jumanne wademocrats walichapisha nyaraka mpya zilizopatikana ambazo zinaonesha mwanasheria binfasi wa rais Trump Rudy Giuliani akifanya kazi na raia wa Ukraine aliyezaliwa Marekani ili kuishinikiza Ukraine kumchunguza Biden.

Kadhalika rais Trump anashtakiwa kwa kuzuia upatikanaji haki kwa kuzuia kutolewa nyaraka muhimu na kuwapiga marufuku mashahidi kuhudhuria vikao vya uchunguzi wa bunge.

Chini ya kanuni ambazo zinahitaji theluthi mbili ya kura za maseneta kuweza kumtoa rais madarakani, Trump anatarajiwa kuondolewa mashtaka yanayomkabili kwa sababu baraza la Seneti linadhibitiwa na chama chake cha Republican.

Hapo jana rais Trump kwa mara nyingine aliukejeli mchakato huo anaoutaja kuwa unaongozwa na wademocrats wanaolenga kumzuia kufanya kazi yoyote.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com