1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yatakiwa kuondoa vikosi vya Jeshi Crimea

8 Desemba 2020

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu limeridhia azimio la kuitaka Urusi kuondoa vikosi vyake vya jeshi Crimea na kufikisha mwisho hatua yake ya kulikalia kwa muda eneo hilo ambalo ni himaya ya Ukraine.

https://p.dw.com/p/3mRBg
Russland | Tag der Marine | Putin kündigt Hyperschallwaffen für Kriegsschiffe an
Picha: Reuters/A. Pavlishak

Wanachama 193 wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa wamepiga kura, huku wanachama 62 wakiliunga mkono azimio hilo la kuitaka Urusi kuondoa vikosi vyake na wengine 17 wakipiga kura ya kulipinga.

Hatua hiyo, ambayo haina mafungamano ya kisheria lakini inaakisi maoni ya ulimwengu, iliungwa mkono na mataifa ya Magharibi na washirika wao na kupingwa na Urusi na washirika wake pamoja na China, Cuba,Venezuela, Iran na Syria.

Urusi ilituma wanajeshi katika eneo la Crimea na kuiteka rasi hiyo mnamo 2014. Imekuwa ikiunga mkono waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine katika kipindi cha miaka sita na kusababisha vita ambavyo vimewaua takriban watu 14,000. Mkataba wa kusitisha mapigano unaosusua umekuwa ukitekelezwa tangu mwishoni mwa Julai. soma zaidi Urusi yaadhimisha miaka mitano tangu kuliteka jimbo la Crimea

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia azimio hilo limelaani vikali uvamizi wa Urusi na ukaliaji wa eneo la Crimea na jiji la Sevastapol na kusisitiza kuwa haliutambua utekaji. Limesisitiza kuwa utekaji kwa nguvu kwa rasi ya Crimea si halali na ni ukiukaji wa sheria za kimataifa, na kuamuru lirudishwe mara moja.

Russland Moskau Siegesparade
Picha: Imago Images

Utekaji kwa nguvu kwa rasi ya Crimea si halali

Hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa imezitolea mwito nchi zote wanachama wa umoja huo na mashirika ya kimataifa kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika kuunga mkono juhudi za kufikisha mwisho ukaliaji wa Urusi wa eneo la Crimea haraka iwezekanavyo.

Aidha Umoja wa Mataifa umesisitiza tena wasiwasi wake mkubwa kuhusu uingizaji wa silaha unaoendelea kufanywa na Urusi na ongezeko la shughuli za kijeshi katika rasi ya Crimea, ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa mifumo ya kisasa ya silaha ikiwemo ndege zenye uwezo wa kubeba silaha za nyuklia na makombora, silaha, risasi na wanajeshi kwenye eneo hilo la Ukraine. Baraza hilo limeitaka Urusi kukomesha shughuli hizo bila kuchelewa. Soma zaidi Ukraine yawazuia wanaume wa Urusi kuingia nchini mwake

Vile vile Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limelaani juhudi za Urusi za kuendelea kuidhalilisha Ukraine na kulidhibiti jeshi lake na kuitaka Urusi kusitisha juhudi zake za kupanua mamlaka kuhusu vifaa vya kinyuklia Crimea, pamoja na kupinga usajili wa wakaazi wa Crimea ikiwa ni pamoja na walio na uraia wa Ukraine. 

Russland Sevastopol Nationalfeiertag Ende WW2 Coronakrise Masken
Picha: picture-alliance/dpa/Sputnik/K. Mihalchevskiy

Hatua ya Urusi kujenga meli za kivita huko Crimea vile vile imepingwa vikali huku Baraza la Umoja wa Mataifa likitoa mwito kwa urusi kujiepusha na ubaharia unaokwenda kinyume na sheria ya kimataifa katika bahari Nyeusi, Bahari ya Azov na mlango wa bahari wa Kerch.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linasema mvutano kati ya Urusi na nchi za magharibi juu ya mzozo huo, wanaendelea kuuzingatia, kama ilivyodhihishwa katika mkutano usio rasmi wiki iliyopita ambapo Urusi ilikutana kujadili juu ya makubaliano ya Minsk kati ya Ukraine na Urusi, ambayo yalifadhiliwa na Ufaransa na Ujerumani.

 

AP/AFPE