1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barack Obama aungwa mkono na John Edwards

P.Martin15 Mei 2008

Nchini Marekani,katika kinyanganyiro cha uchaguzi wa awali kugombea kukiwakilisha chama cha Demokrat katika uchaguzi ujao wa rais baadae mwaka huu,Barack Obama ameungwa mkono na hasimu wake wa zamani John Edwards.

https://p.dw.com/p/E0HY
Democratic presidential hopeful, Sen. Barack Obama, D-Ill., right, is joined by former Democratic presidential hopeful, John Edwards, at a rally in Grand Rapids, Mich., Wednesday, May 14, 2008. (AP Photo/Jae C. Hong)
Barack Obama(kulia) pamoja na John Edwards kwenye mkutano wa Michigan,Mei 14,2008Picha: AP

Jumatano,kwenye mkutano wa hadhara mjini Michigan, John Edwards aliekuwa naibu-rais mteuliwa wa chama cha Demokrat katika mwaka 2004,alimuunga mkono rasmi Barack Obama na hivyo kumuimarisha seneta huyo wa jimbo la Illinois.Edwards aliejitoa tangu mwezi Januari kutoka kinyanganyiro cha uchaguzi wa awali,alipohotubia mkutano wa Michigan alisema,wapiga kura wa Demokrat wameshajiamulia na yeye pia amepitisha uamuzi wake.Akaeleza hivi:

"Kuna mmoja anaejua na kuelewa kuwa huu ni wakati wa kuwa na uongozi ulio thabiti:kuna mmoja anaejua jinsi ya kuleta mageuzi - mageuzi ya kudumu yatakayoanzia tangu chini hadi juu.Kuna mmoja anaejua moyoni mwake kuwa huu ni wakati wa kuunda taifa moja la Marekani na sio mawili.Na mtu huyo ni Barack Obama."

Tangazo hilo ni pigo kwa Hillary Clinton aliesema kuwa ataendelea kugombea kura katika majimbo matano yaliyobaki baada ya kushinda kwa wingi mkubwa katika uchaguzi wa awali hapo Jumanne kwenye jimbo la West Virginia.Katika jimbo hilo Clinton aliungwa mkono na wapiga kura wa kizungu na wale wenye pato dogo. Alijisombea asilimia 67 ya kura kulinganishwa na 26 za Obama na hivyo kuzusha wasi wasi kwa Obama anaejaribu kuwavutia wapiga kura watakaohitajiwa mwezi Novemba ili kuweza kushinda uchaguzi wa rais.

Kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa kwenye tovuti za kujitegemea,Obama sasa ana jumla ya kura 1886 za wajumbe wa chama cha Demokrat wakati Clinton amejikingia kura 1,719.Kwa hivyo Obama anakaribia ile idadi inayohitajiwa yaani 2.025 ili kuweza kuwa mshindi na hivyo kupata nafasi ya kugombea uchaguzi wa rais kwa tikti ya chama cha Demokrat.

Uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa hivi karibuni, umeonyesha kuwa asilimia 60 ya wanachama wa Demokrat wangependa kuona Obama akimchagua Clinton kugombea wadhifa wa makamu wa rais.Lakini wagombea wote wawili wanasema,sasa ni mapema mno kuwa na mazungumzo ya aina hiyo.