1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bangladesh yawahukumu kifo wanamgambo 7 wa shambulio la 2016

Yusra Buwayhid
27 Novemba 2019

Mahakama ya kupambana na ugaidi Bangladesh imewahukumu kifo wanamgambo saba wa kundi lenye misimamo mikali ya kidini Jumatul Mujahedeen, kwa kuhusika na shambulio la mjini Dhaka lilosababisha vifo vya watu 20 mwaka 2016.

https://p.dw.com/p/3TnrJ
Bangladesch angeklagte Islamisten Anschlag auf Holey Artisan Bakery Cafe
Picha: picture-alliance/AP/M.H. Opu

Jaji Mojibur Rahman amewakuta na hatia za mashtaka kadhaa wanamgambo hao wa kundi la kigaidi la Bangladesh la Jumatul Mujahedeen, ikiwamo kupanga shambulio hilo, kutengeneza mabomu pamoja na mauaji. Alitangaza hukumu hiyo mbele ya chumba cha mahakama kilichokuwa kimejaa watu, chini ya ulinzi mkali.

Mnamo Julai mosi mwaka 2016, wanamgambo watano wa kundi hilo la Jumatul Mujahedeen walifyatua silaha katika mgahawa wa Holey Artisan, ambao unapendelewa zaidi na wageni. Watu 20 waliokuwa wameshikiliwa mateka waliuawa ikiwa ni pamoja na raia tisa wa Italia, na saba wa Japan. Afisa wawili wa polisi pia waliuawa. Wanamgambo hao wote watano waliuliwa na makomando wa kijeshi katika makabiliano yaliyodumu kwa zaidi ya masaa 12.

Mwendesha mashtaka wa umma Ghulam Sarwar Khan aliwaambia waandishi wa habari baada ya uamuzi kutolewa katika mji mkuu, Dhaka, kwamba mashtaka dhidi yao yalithibitishwa bila ya shaka yoyote. Na mahakama imewahukumu adhabu kali zaidi. Aliongeza kwamba watu hao saba waliokutikana na hatia Jumatano, walihusika na kupanga shambulio hilo.

Bangladesch Anschlag auf Cafe in Dhaka
Polisi nje ya mgahawa wa Holey Artisan baada ya shambulio mwaka 2016Picha: Reuters/A. Abidi

Kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS lilijaribu kudai kuhusika na shambulio hilo, lakini serikali ya Waziri Mkuu Sheikh Hasina iliyakataa madai hayo, na kusema kwamba kundi la wanmgambo nchini humo ndilo lilohusika.

Mivutano juu ya misimamo mikali ya kidini iliongezeka

Uchunguzi wa polisi umesema shambulio hilo lililenga kulitikisa taifa la Bangladesh, lenye watu milioni 168 wengi wao wakiwa Waislamu.

Shambulio hilo lilichochea mivutano juu ya misimamo mikali wa Waislam nchini humo. Serikali ilizindua kampeni ambapo zaidi ya wanamgambo 100 wa misimamo mikali ya kidini waliuawa na wengine karibu 1,000 kukamatwa.

Kundi la Jamaat-ul-Mujahideen nchini Bangladesh, limenuia kutaka kuanzisha utawala wa sharia za Kiislamu nchini humo.

Baada ya tukio hilo, kulifuatia miaka kadhaa ya mashambulio madogo madogo yaliyolenga watu waliotajwa na wanamgambo hao kuwa ni maadui wa Uislam, ikiwa ni pamoja na wasomi, waandishi, waumini wa dini nyingine za wachache, wageni na wanaharakati.

Uamuzi kamili bado haujatolewa, lakini jaji amesema watu hao walifanya makosa kinyume na uhuru wa nchi pamoja na katiba yake kwa kupanga shambulio kubwa ambalo limelenga na kusababisha vifo vya wageni kadhaa.

Washtakiwa, ambao wameendelea kukana mashtaka hayo kwa kusema hawana hatia, wanaweza kukata rufaa juu ya uamuzi huo.

Vyanzo: (rtre,ap,dpa,afp)