Ban Ki Moon kufanya ziara ya kustukiza mjini Jerusalem | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.10.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ban Ki Moon kufanya ziara ya kustukiza mjini Jerusalem

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon anatarajiwa kufanya ziara ya kustukiza katika maeneo yanayokaliwa na waisrael na wapalestina ikiwa ni jitihada za kukomesha vurugu ambazo zimekuwa zikiendelea .

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon

Ziara hiyo inakuja kufuatia kuendelea kukosekana kwa hali ya utulivu katika eneo hilo kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa baada ya hofu kuzidi kutanda katika mji mtakatifu wa Jerusalem ambao hutumiwa na waumini wa dini zote mbili kiisilamu na kiyahudi kwa ajili ya ibada.

Mapigano ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakiendelea katika eneo hilo yamesaambaa sasa hadi katika maeneo ya jirani yanayokaliwa na waarabu mashariki mwa Jerusalem na baadaye katika ukingo wa magharibi, ukanda wa Gaza na pia Israel.

Hofu yazidi kutanda

Mapigano hayo ya kila siku yamezidi kuleta hofu kiasi cha kuamsha hisia ya kuwa eneo hilo sasa litakuwa linatumbukia katika kipindi kingine cha vurugu nzito.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Palestina Riyad Maliki alikiambia kituo cha radio cha Palestina ya kuwa katibu mkuu Ban Kimoon ambaye kwa sasa yuko barani Ulaya alikuwa anatarajiwa kuwasili baadaye hii leo na kukutana na viongozi wa pande zote mbili ingawa taarifa zaidi kuhusiana na ziara hiyo haikutolewa .

Kwa upande wao Israel walikuwa bado hawajathibitisha rasmi juu ya kuwepo kwa ziara hiyo ya katibu mkuu wa umoja wa mataifa lakini taarifa zinasema ya kuwa balozi mpya wa Israel katika umoja wa mataifa , Danny Danon alikuwa njiani kurejea nyumbani ili kuandaa kikao hicho na waziri mkuu Benjamini Netanyahu. Tayari katibu mkuu Ban Kimoon hapo jana jioni alitoa ujumbe kupitia katika mkanda wa Video akizitaka pande zote mbili kuhakikisha kuwa hali ya utulivu inarejea katika eneo hilo.

Katibu mkuu huyo wa umoja wa mataifa alisema anafahamu vizuri mahitaji ya pande zote mbili lakini akasisitiza ya kuwa vitendo vya vurugu havitakuwa suruhisho la matatizo yao.

Wakati huohuo taarifa za hivi karibuni zinasema ya kuwa mwanajeshi mmoja wa Israel amechomwa kisu katika eneo la ukingo wa magharibi na kuwa mtu ambaye amefanya shambulizi hilo pia ameuawa.

Katika kipindi cha mwezi mmoja waisrael wapatao tisa wameuawa katika mashambulizi ya wapalestina mengi ya hayo yakiwa ya kuchomwa visu, huku wapalestina 41 nao wakiuawa katika mashambulizi ya Israel

Mwandishi: Isaac Gamba/APE/EAP

Mhariri . Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com