1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban Ki-Moon azuru Sudan

3 Septemba 2007

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon leo anaaza ziara ya siku sita nchini Sudan.

https://p.dw.com/p/CH8Z
katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-Moon
katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-MoonPicha: AP

Anatarajiwa kuzindua mpango wa kusuluhisha mzozo wa jimbo la Darfur kwa njia ya mazungumzo na pia swala la kupelekwa wanajeshi wakulinda amani nchini Sudan.

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon ametokea mjini Turin, Italia alikofanya mkutano na maafisa wakuu wa umoja wa mataifa.

Anatarajiwa kuwasilisha mpango wake huo kwa rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan na kumtaka pamoja na serikali yake atoe ushirikiano.

Katibu mkuu anatarajiwa pia kuzuru kambi ya wakimbizi katika jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan.

Huku jimbo la magharibi la Darfur likiwa ndio kiini cha ziara yake ya siku sita katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon atazuru pia eneo la kusini mwa Sudan ambako makubaliano ya kusimamisha mapigano ya mwaka 2005 yanakabiliwa na hali ya wasiwasi,atakutana na rais Silva Kiir wa jimbo hilo la kusini, akiwa katika eneo hilo katibu mkuu atazitembelea nchi jirani za Chad na Libya.

Wiki iliyopita katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon alipendekeza njia tatu za kuutatua mzozo wa jimbo la Darfur, kwanza kupelekwa kikosi cha wanajeshi 26,000 wa kulinda amani wa umoja wa mataifa kwa ushirikiano na kikosi cha wanajeshi na polisi wa umoja wa Afrika kikosi kilichoidhinishwa na baraza la usalama la umoja wa mataifa, pili kufanikisha mazungumzo ya amani yaliyopangiwa kufanyika mwezi Oktoba na tatu kupelekwa misaada.

Ziara hii ya katibu mkuu wa umoja wa mataifa inakwenda sambamba na wimbi jipya la machafuko katika jimbo la Darfur kati ya vikosi vinavyo ungwa mkono na serikali ya Sudan na makundi ya waasi mapigano ambayo maafisa wa umoja wa mataifa wameyataja kuwa yanaongeza hali mbaya ya ukosefu wa chakula kwa raia wa eneo hilo.

Katibu mkuu anatarajiwa kutangaza mahala patakapofanyika mazungumzo hayo ya amani akiwa huko huko nchini Sudan.

Japo kuwa rais Omar el Bashir wa Sudan tangu awali alisema ameridhia kufanyika mazungumzo na pia kupelekwa kikosi cha kulinda amani nchini mwake serikali za magharibi bado zina wasiwasi kufikia kwamba Uingereza na Ufaransa wiki iliyopita zilianzisha mazungumzo wa kuwekewa vikwazo Sudan iwapo haitatoa ushirikiano.

Balozi wa China katika umoja wa mataifa amesema kwamba vikwazo hivyo havitasaidia kutatua matatizo yanayoikabili Sudan.

Katika hatua ya kushangaza kabla ya kuanza ziara ya katibu mkuu, jana Khartoum ilitangaza kuwa inajadili uwezekano wa kumruhusu kurejea nchini humo mkurugenzi wa shirika la kimataifa la kutoa misaada la CARE International ambae nchi hiyo ilimtimua wiki iliyopita kwa madai kuwa anajiingiza katika mambo ya usalama wa ndani wa Sudan, hatua ambayo imepingwa vikali na umoja wa mataifa.

Nchini Chad katibu mkuu atakutana na rais Idriss Deby na watajadili juu ya kupelekwa kikosi cha Umoja wa Ulaya cha kulinda amani kitakacho kuwa na jukumu la kutatua msongamano wa zaidi ya wakimbizi laki mbili waliotoka nchini Sudan.

Ziara ya Ban Ki Moon nchini Libya inalenga kutambua juhudi za rais Muamar Gaddafi za kutafuta suluhisho kati ya makundi mawili yale yanayoungwa mkono na serikali na waasi yanayozozana nchini Sudan.