1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Balozi wa Ufaransa aondoka Niger

27 Septemba 2023

Balozi wa Ufaransa nchini Niger Sylvain Itte ameondoka mjini Niamey mapema Jumatano asubuhi.

https://p.dw.com/p/4Wr7s
Französischer Diplomat Sylvain Itte
Aliyekuwa Balozi wa Ufaransa nchini Niger Sylvain IttePicha: Hugo Ortuño/picture alliance/dpa/EPA

Hayo yameelezwa na vyanzo viwili vya usalama, ikiwa ni karibu mwezi mmoja tangu utawala wa kijeshi wa Niger kuamuru aondoke mara moja nchini humo.

Wanajeshi walionyakua mamlaka katika mapinduzi ya Julai 26 huko Niger, waliamuru Agosti 25 kuwa Balozi wa Ufaransa nchini humo Sylvain Itte alipaswa kuondoka nchini humo ndani ya masaa 48, ikiwa kama jibu kwa kile walichosema ni vitendo vya Ufaransa vilivyo "kinyume na  maslahi ya Niger".

Lakini agizo hilo hapo awali lilipuuzwa na Ufaransa, ambayo ilikataa kuwatambua viongozi hao wa kijeshi, na hivyo kusababisha maandamano ya kila siku mbele ya Ubalozi wa Ufaransa mjini Niamey. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alibaini mwezi huu kwamba Balozi Itte na wasaidizi wake walikuwa wakishikiliwa mateka ndani ya ubalozi huo.

Supporters of the military administration in Niger storm French air base
Raia wa Niger wakiandamana kuwaunga mkono wanajeshi waliofanya mapinduzi na kutaka Balozi wa Ufaransa kuondoka nchini humo:25.08.2023Picha: Balima Boureima/AA/picture alliance

Mara kadhaa Macron amekuwa akisisitiza kwamba Ufaransa isingelibadilisha msimamo wake wa kuyalaani mapinduzi hayo ya kijeshi na kuahidi kumsaidia rais aliyepinduliwa, Mohamed Bazoum, akisisitiza kwamba ndiye aliyechaguliwa kidemokrasia na kwamba alikuwa jasiri kwa kukataa kujiuzulu.

Mwishoni mwa wiki iliyopita,  Rais Macron  alitangaza kuwa Ufaransa imechukua uamuzi wa kuwaondoa wanajeshi wapatao 1,500 pamoja na Balozi wake nchini Niger. Katika mahojiano maalumu kupitia televisheni ya Ufaransa, pasipo kutoa ufafanuzi wa kina, Macron alisikika akisema Ufaransa imeamua kumuondoa balozi wake katika kipindi cha masaa kadhaa yajayo lakini pia wanadiplomasia wake kadhaa watarejea nyumbani.

Aliongeza kuwa ushirikiano wa kijeshi "umekwisha" na wanajeshi wa Ufaransa watajiondoa katika miezi na wiki zijazo, na kwamba suala la kujiondoa kikamilifu litafikiwa "mwishoni mwa mwaka". Aidha Macron alisema walikuwa katika ardhi ya Niger kwa ombi la Burkina Faso na Mali.

Paris Macron und Mohamed Bazoum Präsident von Niger
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kushoto) akimpokea Aliyekuwa Rais wa Niger Mohamed Bazoum katika Ikulu ya Elysée mjini Paris: 16.02.2023Picha: Michel Euler/AP/picture alliance

Rais huyo wa Ufaransa  alisisitiza kuwa operesheni ya kijeshi iliyopewa jina "Barkhane" , imekuwa ya mafanikio na kwamba bila ya operesheni hiyo, nchi nyingi kati ya hizo (akimaanisha katika ukanda wa Sahel), zingekuwa tayari zimechukuliwa na makundi yenye itikadi kali.

Wananchi wa Niger wamepokea vyema taarifa hii ya kuondoka kwa Balozi wa Ufaransa nchini mwao. Tanko Karim mkazi wa Niamey amesema:

" Tumepata ushindi dhidi ya Ufaransa na ukoloni mamboleo. Kwa hakika, kuondoka kwa Balozi Itté ni ushindi.”

Tangazo hilo lilipokelewa pia vyema na viongozi wa kijeshi wa Niger waliosema ni hatua njema kuelekea uhuru wa taifa lao, na kuongeza pia huu ni wakati wa kihistoria, ambao unaelezea hisia za watu wa Niger.

(Vyanzo: RTRE, AFPE)