Balozi wa Myanmar nchini Uingereza atimuliwa ofisini | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.04.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Balozi wa Myanmar nchini Uingereza atimuliwa ofisini

Balozi wa Myanmar nchini Uingereza, ambaye amekosoa mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa nchini mwake, amesema amefungiwa nje ya ofisi yake iliyoko mjini London na nafasi yake kuchukuliwa na naibu wake.

Balozi wa Myanmar nchini Uingereza, ambaye amekosoa mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa nchini mwake, amesema amefungiwa nje ya ofisi yake iliyoko mjini London na nafasi yake kuchukuliwa na naibu wake. 

Kyaw Zwar Minn amesema amezuiliwa kuingia kwenye ofisi ya ubalozi wake jana Jumatano na wanadiplomasia ambao ni watiifu kwa utawala wa jeshi nchini Myanmar.

Ameliambia gazeti la Uingereza la The Daily Telegraph, na hapa namnukuu: "Wamekataa kuniruhusu niingie kwenye ofisi yangu. Wamesema wamepokea agizo kutoka mji mkuu, kwa hiyo hawawezi kuniruhusu niingie.” Mwisho wa nukuu.

Balozi huyo ameitaja hatua hiyo ya kumzuia kuingia ofisini mwake kama "mapinduzi”.

"Hii nafkiri munajua, sio Burma. Hii ni London. Ndio, wameuzingira ubalozi wangu. Hapana, Hapana, sina raha."

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Dominic Raab leo alhamisi amelaani kile alichokiita vitendo vya uonevu vya utawala wa jeshi la Myanmar. Raab amesifu ujasiri wa balozi huyo wa Myanmar nchini Uingereza.

Hata hivyo, haijakuwa bayana iwapo Uingereza inaweza kuchukua hatua yoyote juu ya tukio hilo.

Maandamano yanazidi kushika kasi baada ya mapinduzi ya kijeshi

Mwezi uliopita, balozi huyo alitoa wito wa kuachiliwa huru kwa kiongozi wa Myanmar aliyechaguliwa kidemokrasia Aung San Suu Kyi, ambaye amewekwa kizuizini tangu jeshi lilipochukua madaraka mnamo Februari, 1.

Katika barua iliyotumwa kwa wizara ya mambo ya nje ya Uingereza kutoka makao makuu ya Myanmar, ambayo imeonekana na shirika la habari la Reuters, inasema kuwa naibu balozi Chit Win sasa ndiye amechukua nafasi hiyo kuanzia Aprili 7 na kuwa Kyaw Zwar Minn alitakuwa kurudi nyumbani mnamo Machi, 9.

Kyaw kupitia msemaji wake, amesema kuwa ana imani kwa serikali ya Uingereza kuwa itaendelea kupinga utawala haramu wa kijeshi nchini Myanmar.

Wakati hayo yakiarifiwa, maandamano yameendelea kushika kasi nchini Myanmar. Waandamanaji wanaopinga mapinduzi ya kijeshi wamekabiliana na vikosi vya usalama katika mji wa kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, Taze.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti leo Alhamisi kuwa waandamanaji wasiopungua 11 wameuawa na wengine 20 wamejeruhiwa katika patashika hiyo kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji.

Mauaji ya leo yanafikisha idadi jumla ya zaidi ya watu 600 waliouawa tangu jeshi lilipochukua madaraka mnamo Februari, 1.