BAGHDAD: Yamkini Rais wa zamani wa Iraq akanyongwa kesho. | Habari za Ulimwengu | DW | 29.12.2006
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

BAGHDAD: Yamkini Rais wa zamani wa Iraq akanyongwa kesho.

Haijafahamika wazi wazi siku ambayo rais wa zamani wa Iraq Saddam Hussein atanyongwa.

Wakili wa Saddam amewaambia waandishi wa habari kwamba ametakiwa kwenda kupokea vitu vya matumizi ya binafsi vya mteja wake, hatua ambayo inaashiria kwa vyovyote vile kiongozi huyo wa zamani atatiwa kitanzi.

Najib Aal-Nuami, wakili wa Saddam ambaye alikuwa waziri wa zamani wa sheria wa Qatar amesema huenda adhabu dhidi ya Saddam Hussein ikatekelezwa kesho.

"Nimeambiwa na mmoja wa mawakili wetu kwamba alikutana na Saddam Hussein jana. Anasema dalili zinaashiria huenda Saddam akanyongwa kesho. Nadhani Wamarekani hawatamkabidhi kwa Iraq. Huenda wataandamana naye hadi mwisho"

Waziri Mkuu Nouri Al-Maliki amesema hakuna lolote litakalozuia au kuchelewesha kutekelezwa adhabu hiyo.

Hata hivyo, afisa mkuu wa wizara ya sheria amesema hukumu hiyo haitatekelezwa kabla ya tarehe 26 mwezi ujao, ambayo itakuwa mwezi mmoja tangu mahakama ya Iraq ilipomhukumu Saddam adhabu ya kifo.

Mtawala huyo wa zamani wa kiimla alihukumiwa adhabu ya kifo kwa mauaji ya mwaka elfu moja mia tisa themanini na mbili ya watu takriban mia moja na hamsini katika mji wa Dujail, ambao wakazi wake wengi ni wa jamii ya kishia.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com