1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD: Wanajeshi wa Uingereza na Marekani waendelea kupata maafa nchini Iraq.

21 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCZ8

Askari mmoja wa Uingereza ameuawa na wengine wanne wakajeruhiwa karibu na mji wa Basra, kusini mwa Iraq.

Msemaji wa majeshi ya Uingereza amesema mmoja wa wanajeshi waliojeruhiwa yumo katika hali mahututi.

Shambulio hilo limetokea wakati ambapo idadi ya askari wa Marekani waliouawa nchini Iraq imeongezeka baada ya vifo vya watu ishirini na mmoja.

Helikopta ya kijeshi ya Marekani ilianguka jana kaskazini mashariki mwa Baghdad na kusababisha vifo vya askari kumi na watatu.

Majeshi ya Marekani yamesema sababu ya ajali hiyo haijajulikana.

Saa chache baadaye, askari wengine watano wa Marekani waliuawa na wengine watatu wakarejuhiwa kwenye mapambano kati yao na wanamgambo katika mji mtakatifu wa kishia wa Karbala, kusini mwa Iraq.

Askari mwengine aliuawa kwenye mripuko wa bomu lililotegwa barabarani mjini Baghdad.

Wanajeshi wengine wawili waliuawa siku ya Ijumaa.

Majeshi ya Marekani yamepata pigo hilo huku askari wa mwanzo miongoni mwa wanajeshi elfu ishirini na moja wa ziada wakianza kuwasili nchini Iraq.

Wanajeshi hao wamepelekwa Iraq kufuatana na mpango wa Rais George W. Bush, kuwapeleka wanajeshi ya ziada nchini Iraq.