BAGHDAD : Saddam ahukumiwa kunyongwa | Habari za Ulimwengu | DW | 05.11.2006
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

BAGHDAD : Saddam ahukumiwa kunyongwa

Mahkama Kuu ya Iraq inayoungwa mkono na Marelani imehukumu kifo kwa kunyongwa Saddam Hussein kwa kumuona na hatia ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu kwa kule kuamuru kuuwawa kwa raia wa madhehebu ya Shia 148 kufuatia jaribio dhidi ya maisha yake hapo mwaka 1982 katika kijiji cha Dujail.

Rais huyo wa zamani wa Iraq alionekana kufadhaika na kutamka na Mungu Mkubwa.Baada ya hukumu hiyo kusomwa Saddam aliekuwa akitetemeka aliwapomgeza wananchi wake na kulaani wasaliti wa Iraq.

Kaka yake wa kambo na mkuu wa zamani wa ujasusi Barzan Ibrahim al Takriti na Awad Hamed al Bandar mkuu wa zamani wa mahkama ya kimapinduzi pia wamehukumiwa kifo kwa kunyongwa.

Makamo wa rais wa zamani Taha Yassin Ramadhan amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

Maafisa wengine watatu wa zamani wa chama cha Baath wamehukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani kwa dhima waliyotimiza katika mauaji hayo ya Washia.Afisa mwengine mmoja ameachiliwa huru.

Hukumu ya kifo au kifungo cha maisha moja kwa moja huingia katika rufaa na hiyo kukawilisha utekelezaji wake kwa miezi kadhaa.

Saddam mwenyewe alikuwa akitaka hukumu hiyo ikiwa ya kifo iwe kwa kupigwa risasi na sio kwa kunyongwa.

Muda mfupi baada ya kutangazwa kwa hukumu hiyo kulizuka mapambano kati ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Iraq katika vitongoji viwili vya Sunni karibu na mji mkuu wa Baghdad.

Washia ambao hivi sasa ndio wenye kuidhibiti Iraq walimininika mitaani kushangilia hukumu hiyo dhidi ya dikteta aliyewakandamiza kwa miongo mitatu.

Wasunni katika mji Tikrit alikozaliwa Saddam alitoka mitaani na kufyetuwa risasi hewani kulaani hukumu hiyo.

Timu ya mawakili wanaomtetea Saddam wamesema hukumu hiyo ni kuidhihaki sheria na kwamba sio halali na ya kisiasa.

Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al Maliki akiipongeza hukumu hiyo amesema kunyongwa kwa Saddam hakuwezi kulinganishwa na tone moja la damu ya mashahidi waliopoteza maisha yao wakipinga utawala wake.

Amesema hukumu hiyo ni ushindi kwa wahanga wa utawala wa Saddam na mwisho wa enzi ya vitisho.

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com