BAGHDAD : Saddam ahukumiwa kifo kwa kunyongwa | Habari za Ulimwengu | DW | 05.11.2006
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

BAGHDAD : Saddam ahukumiwa kifo kwa kunyongwa

Mahkama Kuu ya Iraq leo imemhukumu kifo kwa kunyongwa Saddam Hussein kwa kumuona na hatia ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu kwa kule kuamuru kuuwawa kwa raia wa madhehebu ya Shia 148 kufuatia jaribio dhidi ya maisha yake hapo mwaka 1982 huko Dujail.

Rais huyo wa zamani wa Iraq alionekana kufadhaika na kutamka Mungu Mkubwa.Baada ya hukumu hiyo kusomwa Saddam aliekuwa akitetemeka alipiga mayowe akitamka Lidumu taifa adhimu na kifo kwa wasaliti wa Iraq.

Kaka yake wa kambo na mkuu wa zamani wa ujasusi Barzan Ibrahim al- Takriti na Awad Hamed al Bandar mkuu wa mahkama ya kimapinduzi pia wamehukumiwa kifo kwa kunyongwa.

Makamo wa rais wa zamani Taha Yassin Ramadhan amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

Maafisa wengine watatu wa zamani wa chama cha Baath wamehukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani kwa dhima waliyotimiza katika mauaji hayo.Afisa mwengine mmoja ameachiliwa huru.

Saddam Hussein mwenyewe alikuwa akitaka hukumu hiyo ya kifo iwapo atahukumiwa hivyo iwe kwa kupigwa risasi na sio kitanzi.

Mji mkuu wa Baghdad uko katika ulinzi mkali wakati mahkama hiyo ilipokuwa ikitowa hukumu yake hiyo dhidi ya dikteta wa zamani wa nchi hiyo na washtakiwa wenzake saba.

Serikali ya Iraq inahofu kwamba wafuasi wa kiongozi huyo aliepinduliwa watafanya mashambulizi iwapo Saddam atahukumiwa kifo katika kesi yake hiyo ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu.Kuanzia mapema leo asubuhi barabara zote zimefungwa kwa waendao kwa miguu na magari halikadhalika hadi hapo itakapotolewa taarifa zaidi na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Baghdad pia umefungwa.

Jeshi la nchi hiyo limejiandaa kwa vita na amri ya kutotoka nje kabisa imewekwa katika majimbo matatu ya vurugu ukiwemo mji mkuu wa Baghdad na miji miwili yenye mapambano ya kimadhehebu ya Diyala na Tikrit alikozaliwa Saddam.

Wakati huo huo takriban watu 30 wameuwawa hapo jana katika mashambulizi ya wanamgambo nchini kote Iraq.

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com