1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD : Mapambano na jeshi la Mehdi yazuka tena

27 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBxr

Wanajeshi wa Marekani na Uingereza wamepambana na jeshi la Mehdi katika mji wa Baghdad na Basra hapo jana.

Kuzuka upya kwa mapigano hayo kumekuja baada ya kiongozi wa jeshi hilo la Mehdi sheikh wa Kishia Moqtada al Sadr kutumia kujitokeza kwake hadharani kwa nadra kwa wito wa kutaka wanajeshi wa Marekani waondoke nchini Iraq.

Wapiganaji watano wameuwawa katika shambulio la anga wakati wa alfajiri hapo jana katika mji ulio ngome kuu kwa sheikh huyo wa Sadr ulioko Baghdad.Hata hivyo afisa wa ulinzi wa Iraq amesema kwamba shambulio hilo la anga kwa ajili ya kusaidia shambulio la ardhini limepiga magari yaliokuwa katika msururu wa kununuwa mafuta na kwamba waliouwawa walikuwa ni raia wasiokuwa na hatia.

Katika mji wa kusini wa Basra jeshi la Uingereza limesema wanamgambo kadhaa wameuwawa katika shambulio la anga wakati wa usiku baada ya kuwashambulia wanajeshi wa Uingereza kwa maroketi,mizinga na bunduki za rashasha.

Wakati huo huo imefahamika kwamba wanajeshi wanane wa Marekani wameuwawa katika mashambulizi mbali mbali katika kipindi cha siku nne na kufanya idadi ya wanajeshi wa Marekani waliouwawa katika mwezi wa Mei hadi sasa kufikia 101.

Mwezi wa April ulikuwa wa maafa makubwa kwa wanajeshi wa Marekani ambapo jumla ya wanajeshi 104 waliuwawa.