1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD : Brown apinga uchunguzi wa vita Iraq

12 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBsX

Waziri Mkuu mteule wa Uingereza Gordon Brown yuko nchini Iraq kwa kile maafisa wa serikali yake wanachosema ni ziara ya kutafuta ukweli ambayo imejumuisha mazungumzo na Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al- Maliki.

Ziara yake hiyo inakuja wakati kukiongezeka wito kutoka kwa chama cha upinzani cha Conservative nchini Uingereza wa kuanzishwa uchunguzi rasmi juu ya namna serikali ilivyoshughulikia vita vilivyoongozwa na Marekani nchini Iraq.

Akipinga wito huo Brown ambaye ni waziri wa fedha anayetarajiwa kuchukuwa nafasi ya Tony Blair mwishoni mwa mwezi huu amesema kipau mbele cha kwanza ni kuyasaidia majeshi yalioko nchini Iraq.

Brown amesema tayari wamepunguza idadi ya wanajeshi wao nchini Iraq lakini wana wajibu na wamewaahidi wananchi wa Iraq wajibu walioahidi kutimiza pamoja na nchi nyengine kwa kupitia Umoja wa Mataifa.

Wakati Brown akikataa wito huo wa uchunguzi kutokana na kuwa sio wakati muafaka hakufuta uwezekano wa kufanyika kwa uchunguzi huo hapo baadae.