1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bado kuna wanasiasa wachache wa kike Ujerumani

Iddi Ssessanga
23 Agosti 2017

Angela Merkel ameongoza serikali kuu ya Ujerumani kwa miaka kadhaa. Lakini watunga sera wa kike wanazidi kupungua. Ukiwa huna familia lazima ujithibitishe, na hata mwenye watoto vivyo hivyo. Ni mashaka.

https://p.dw.com/p/2iifJ
Symbolbild Frauenquote Politikerinnen
Picha: picture-alliance/dpa/S. Stache

"Mabibi na Mabwana": Maneno haya yanayoonekana kuwa ya kawaida ndiyo yalianza hotuba katika bunge la taifa la Weimer Februari 19, 1919, ambayo ilikuja kuwa sehemu ya historia, pia kutokana na maudhui yake, lakini hasa kwa sababu maneno hayo yalitoka kwenye kinywa cha mwanamke. Marie Juchacz alikuwa mwanasiasa wa kwanza wa kike kuzungumza mbele ya bunge lililochaguliwa kidemokrasia nchini Ujerumani. Hii ilikuwa miezi mitatu tu tangu kupitishwa kwa sheria ya haki ya wanawake kupiga kura.

Juchacz, mwanasiasa wa chama cha SPDn alikuwa mmoja wa wanawake 37 walioingia bungeni mwaka 1919, ambao walichangia karibu asilimia tisa ya wabunge wote. Leo hii, karibu miaka 100 baadae idadi ya wanawake katika bunge la Ujerumani Bundestaga ni asilimia 37.1, hii ikimaanisha kuwa bado hawajapata uwakilishi wa kutosha katika uwanja wa kisiasa nchini humo. Katika orodha ya kimataifa kuhusu uwakilishi wa wanawake, Ujerumani inashika nafasi ya 22 kati ya mataifa 190, na kulingana na utafiti mpya wa maoni kuelekea uchaguzi mkuu wa Septemba, hali inaweza kuwa mbaya zaidi, kutokana na uwezekano wa kiwango cha uwakilishi wao kushuka hadi asilimia 32.

Wahlkampf der CDU Niedersachsen mit Angela Merkel
Merkel ameongoza serikali kuu ya Ujerumani kwa miaka kadhaa, lakini idadi ya wanasiasa wanawake bado ni ndogo.Picha: picture alliance/dpa/P. Steffen

Watoto watatu, na kazi kwa saa 80 kwa wiki

Swali ni je, hii inataokana na ukweli kwamba hawataki, au ni vigumu zaidi kwa wanawake kuifanya siasa kama kazi yao kuu? Dorothee Bär kutoka chama cha Christian Social Union CSU, ambaye ni mjumbe wa bunge la sasa la shirikisho, anaamini kuwa wanawake wanahitaji kudhihirisha zaidi uwezo zao na kujithibitisha. Wenzao vijana walio na watoto wanatazamwa kwa jicho la ukosoaji na hawachukuliwi kwa uzito. Na ikiwa mwanasiasa wa kike ana mtoto, pia atahesabiwa kuwa mwenye hasara.

Bär ana watoto watatu na anafanya kazi kwa saa kati ya 70 na 80 kwa wiki. Anapokuwa kwenye vikao vya bunge bila familia mjini Berlin, kazi inaweza kuwa kubwa bado, "sina muda wa kumpuzika hata jioni", anasema mwanasiasa huyo. Wengi wa marafiki zake wana watoto wadogo kama ilivyo kwake na kazi ya nusu siku. Lakini kazi ya siasa aghalabu ni ya siku nzima na Bär anasema, wanawake wengi hawataki kazi ya namna hiyo.

Wanawake zaidi kwa mafanikio zaidi

Vyama vya muungano vya CDU na CDU vina uwakilishi wa wanawake 79 tu ikilinganishwa na wanaume 230. Hata naibu mwenyekiti wa chama cha CSU Barbara Stamm anazungumzia pengo kubwa kati ya wanaume na wanawake ndani ya uongozi wa chama. Stamm anasema chama laazima kifahamu kwamba ili kuwa na mustakabali mwema, laazima kuwepo na ulinganifu katika uwakilishi wa wanaume na wanawake. Hayo lakini, tayari vyama vingine vimeyatekeleza. Vyama vya Kijani na kile cha mrengo wa kushoto Die Linke vinawakilishwa na wanawake wengi zaidi kuliko wanaume.

Flash-Galerie Konstituierende Sitzung Bayerischer Landtag
Naibu mwenyekiti wa CSU Barbara Stamm, anaamini vyama vinapaswa kusawazisha uwakilishi wa wanawake na wanaume ili kuwa na mustakabali bora.Picha: picture-alliance/dpa

Kwa mfano, mtaalamu wa sayansi ya siasa kutoka chuo kikuu cha Münster Wichard Woyke, anazumgumzia mwanasiasa wa chama cha SPD Hannelore Kraft alivyokifufua chama hicho katika jimbo la North-Rheine Westpahalia baada ya kupoteza uungwaji mkono katika uchaguzi wa mwaka 2005. Bibi Kraft alianza kwa kuchukuwa uongozi wa kundi la wawakilishi wa chama hicho katika bunge la jimbo, na baadae akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama wa jimbo, na mwaka 2010 waziri mkuu wa jimbo.

Suala la madaraka na mazingira ya kazi

Kwa mujibu wa Woyke, kuchanganya familia na siasa ni vitu viwili visivyowiana katika mipango ya muda mrefu, isipokuwa kama unaye mume anaekubali kuwa mume wa nyumbani na ashughulikie masuala yote ya watoto, hili linawezekana baadhi ya wakati lakini la nadra. Lakini pia lipo suala la madaraka. Ni jambo ambalo wanawake wengi wasingependelea kulizungumzia, anasema Bär.

Lakini licha ya yote hayo, inafaa kwa mwanamke kujitosa katika siasa kwa sababu wanawake wana njia tofauti za kushughulikia masuala mbalimbali, hasa yanayowahusu wanawake wenzao, ambayo wanaume hawana majibu yake.

Mwandishi: Nastassja Shtrauchler/DW Nachrichten

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Josephat Charo