Bado de Maiziere yu mashakani | Magazetini | DW | 24.07.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Bado de Maiziere yu mashakani

Wahariri wanazungumzia sakata la ndege zisizokuwa na rubani linalomkabili Waziri wa Ulinzi, Thomas de Maiziere, ziara ya Baba Mtakatifu Francis nchini Brazil na umuhimu wa wanafunzi mashuleni kutumia mitandao ya kijamii.

Bundesverteidigungsminister Thomas de Maiziere (CDU) spricht am 05.06.2013 in der Bundespressekonferenz in Berlin nach der Sitzung des Verteidigungsausschusses des Bundestages. Foto: Maurizio Gambarini/dpa +++(c) dpa - Bildfunk+++

Thomas de Maiziere Verteidigungsminister Verteidigungsausschuss PK 05. Juni 2013

Mhariri wa Neue Osnabrücker, ambaye ameguswa na ya Waziri de Maiziere, anasema ni vigumu sana mwanasiasa huyo kupona mbele ya Tume ya Uchunguzi juu ya kadhia ya ndege zisizo rubani, anasema mhariri huyo.

Tume hiyo ya bunge inaweza kabisa kumtia hatiani de Maiziere kwa kudanganya kwamba alikuwa hajui kuwa kile kiitwacho "Euro Hawk" ulikuwa mradi wenye utata.

Mhariri anasema kwamba chochote kiwacho, ama kama alikuwa hajui au kama alidanganya, yote ni makosa yanayotosha kumfanya awajibike.

Papa Francis nchini Brazil: mchanganyiko wa picha

Baba Mtakatifu Francis akiwa ziarani Brazil.

Baba Mtakatifu Francis akiwa ziarani Brazil.

Mhariri wa Westfalen-Blatt anazungumzia ziara ya mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Francis, nchini Brazil, akisema kwamba imeshuhudia mchanganyiko wa vurugu na mapenzi ya watu kwake.

Hizi ni picha mbili zinazosutana lakini zinaisawiri ziara hii. Upande mmoja wananchi wana hasira na serikali yao, kwa sababu ya ugumu wa maisha, lakini kwa upande mwengine, kuna ufuasi mkubwa wa Wabrazil kwa kanisa hilo, na mapenzi yao mahsusi hasa kwa Baba Francis, ambaye amejipambanua kama Papa wa wanyonge.

Naye, badala ya kuzingatia onyo la walinzi wake kwamba hali si salama sana kwenye halaiki, yeye aliwakaribia, akawashika mikono, akawabusu, na baadhi ya wakati hata kuwakumbatia watu wa kawaida mitaani.

Kodi ya kadi ya mkopo

Kadi ya mkopo, Mastercard.

Kadi ya mkopo, Mastercard.

Kodi ya kadi za mkopo barani Ulaya sasa imeshadhihirika wazi kwamba ni tatizo kubwa, anasema mhariri wa Stuttgarter Zeitung, kwani wafanyabiashara na wanunuzi wa kawaida, watajikuta sasa wanakatwa zaidi ya kile wanachokinunua.

Hatua za Brussels kujaribu kudhibiti fedha za Ulaya zisitoweke kwenye makasha ya hazina zake, hazieleweki. Kwa kupitisha kodi hiyo, maana yake ni kwamba unawafanya wateja wa kadi hizo waamue kuzirejesha, na hivyo wasikope, na hivyo matumizi yasifanyike na, hatimaye, pesa isizunguke.

Mhariri huyo anauiita huu kuwa ni mduara wa papo kwa papo wa madeni, hasara, na mporomoko wa kiuchumi. Kama Ulaya haijaona njia ya kujikwamua kutoka mzozo wake wa sarafu ya euro, basi hii ya sasa ni njia ya kuirudisha kinyumenyume, anaonya mhariri.

Facebook na wanafunzi

Alama za mitandao ya Facebook na Instagram.

Alama za mitandao ya Facebook na Instagram.

Mhariri wa Rheinische Post anahoji juu ya haja ya wanafunzi mashuleni kuruhusiwa kutumia mitandao ya kijamii, kama vile Facebook, hasa kwenye jimbo la North-Rhine Westphalia.

"Tunaweza kukataa mengi, lakini si ukweli kwamba Facebook imekuwa sehemu muhimu ya maisha ya skuli, hasa kwa vijana wetu", anasema mhariri huyo.

Kwa hivyo, wakosoaji wako sahihi, pale wanapopinga hatua za walimu kuwatenganisha wanafunzi na mfumo huu wenye taarifa nyingi zaidi, pengine kuliko hata vitabu vyao. Maana, kwa hakika, hilo si jambo linalowezekana.

Ni kweli kwamba kuna masuala ya kisheria, kama vile sheria inayowazuia watoto kuangalia “mambo ya kijitu kizima“, lakini hilo linaweza kushughulikiwa zaidi kwa miongozo na mafunzo kuliko kupiga marufuku.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Vyanzo: Neue Osnabrücker, Westfalen-Blatt, Stuttgarter Zeitung, Rheinische Post
Mhariri: Saumu Yusuf