Baba Mtakatifu aunga mkono kuundwa kwa dola huru la Wapalestina | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 13.05.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Baba Mtakatifu aunga mkono kuundwa kwa dola huru la Wapalestina

Baba Mtakatifu Benedict XVI ataka kuzingirwa kwa Ukanda wa Gaza kumalizike.

Baba Mtakatifu Benedict XVI akiusalimia umati wa watu nje ya kanisa la Bethlehemu

Baba Mtakatifu Benedict XVI akiusalimia umati wa watu nje ya kanisa la Bethlehemu

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Benedict XVI ameutembelea mji wa Bethlehemu ulio katika Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan. Akiwa mjini humo kiongozi huyo ametangaza kwamba makao makuu ya kanisa Katoliki, Vatican, yanaunga mkono kuundwa kwa dola huru la Palestina litakalokaa kwa amani na Israel.

Akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake nchini Israel, Baba Mtakatifu Benedict VXI amesafiri kwenda mji wa Bethlehemu kupitia ukuta wa usalama wa Israel unaoutenganisha mji huo na mji wa Jerusalem. Mjini Bethlehemu amelakiwa na mwenyeji wake rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas, ambaye ameulaani ukuta wa Israel akiutaja kuwa wa kibaguzi na sehemu ya juhudi za taifa hilo la kiyahudi kuwafukuza Wapalestina Wakristo na Waislamu. Rais Abbas ameilaani hatua ya Israel kuyakalia maeneo ya Wapalestina kwa miaka 42 na hatua ya kuwazuia Wapalestina kutembea kwa uhuru katika ardhi yao.


Papa Benedict VXI amerudia tena msimamo wa makao makuu ya kanisa Katoliki kuunga mkono suluhu ya kuundwa taifa huru la Wapalestina katika kuutanzua mzozo kati ya Israel na Wapalestina. Suluhu hiyo inaungwa mkono na rais Mahmoud Abbas na nchi za magharibi, lakini waziri mkuu wa sasa wa Israe, Benjamin Netanyahu amekuwa akisita. Hata hivyo Baba Mtakatifu amemtaka rais Abbas asivunjike moyo.

"Ingawa lengo hili bado lingali mbali kufikiwa, nakuhimiza wewe pamoja na watu wako kuendelea kuwa na matumaini."

Palästinenserpräsident Abbas will Referendum zu Unabhängigkeit

Rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina Mahmoud Abbas

Kiongozi huyo amesema anafahamu ni kwa kiasi gani Wapalestina walivyoteseka na wanavyoendelea kuteseka kutokana na machafuko yaliyolikabili eneo hilo kwa miongo kadhaa. Amesema anazihurumia jamii zote zilizopoteza mali na wapendwa wao na kusema Wapalestina bado hawajasahauliwa.

"Natumai kuja kwangu hapa ni ishara kwamba hamjasahaulika na kwamba uvumilivu wenu kuwa hapa na kudumu kwenu katika imani ni muhimu machoni pa Mungu."

Baba Mtakatifu pia amesema ataitembelea kambi ya wakimbizi ya Aida nje ya mji wa Bethlehemu ambako wakimbizi takriban 4,600 wanaishi. Wakimbizi hao waliyakimbia makazi yao ambayo sasa ni sehemu ya Israel wakati taifa hilo lilipoundwa mnamo mwaka 1947. Wana matumaini kwamba kiongozi huyo wa kanisa Katoliki duniani atauhamasisha ulimwengu kuhusu madai yao ya kutaka kurejea katika vijiji vyao 43 ambavyo wao na mababu zao walikuwa wakiishi. Madai hayo hata hivyo yanapingwa na Israel.

Papa Benedict XVI ameitaka jumuiya ya kimataifa kutumia ushawishi wake kuumalizi mzozo wa Mashariki ya Kati. Amewatolea mwito vijana katika maeneo ya Wapalestina wasiwe na uchungu wala chuki mioyoni mwao kutokana na uharibifu na kuwapoteza jamaa zao katika vita dhidi ya Ukanda wa Gaza. Amewataka vijana hao waepuke majaribu ya kutaka kulipiza kisasi, wasigeukie machafuko wala kujiingiza katika vitendo vya kigaidi.

Bildgalerie Heilige Stätten Geburtskirche Bethlehem Flash-Galerie

Kanisa la Bethlehem lililojengwa mahala ambapo Yesu Kristo alizaliwa kwenye zizi la ng´ombe

Baba Mtakatifu ameongoza misa katika uwanja wa Manger, nje kidogo na kanisa moja mjini Bethlehemu. Maelefu ya watu walikusanyika katika uwanja huo ambao Wakristo wanaamini Yesu Kristo alizaliwa kwenye hori la ng´ombe.

Papa Benedict VXI amewaambia waumuni kwenye misa hiyo kwamba anaombea kuondolewa kwa hatua ya Israel kuuzingira Ukanda wa Gaza, iliyoanza kutekelezwa mnamo mwezi Juni mwaka 2007 wakati chama cha Hamas kilipotwaa madaraka katika Ukanda wa Gaza na kuapa kuliangamiza taifa hilo la kiyahudi.

Mwandishi: Josephat Charo/AFP/RTRE

Mhariri: Thelma Mwadzaya

 • Tarehe 13.05.2009
 • Mwandishi Charo Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Hp9C
 • Tarehe 13.05.2009
 • Mwandishi Charo Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Hp9C
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com