1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baba Mtakatifu akamilisha ziara yake Ujerumani

26 Septemba 2011

Ndege ya shirika la Lufthansa iliyombeba papa Benedict XVI ilitua katika uwanja wa ndege wa Ciampino mjini Roma jana usiku ikitokea Lahr, Ujerumani.

https://p.dw.com/p/12gIs
Papa Benedikt XVIPicha: dapd

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Benedict XVI, amerejea Roma baada ya kukamilisha ziara yake ya siku nne hapa Ujerumani. Ndege iliyombeba kiongozi huyo ya shirika la ndege la Ujerumani, Lufthansa, ilitua katika uwanja wa ndege wa Ciampino mjini Roma mwendo wa saa tatu kasorobo usiku ikitokea mji wa Lahr Ujerumani.

Papst Papstbesuch 2011 Freiburg
Baba Mtakatifu akiondoka Lahr, kaskazini mwa Freiburg.Picha: dapd

Papa alisindikizwa na rais wa Ujerumani, Christian Wulff, katika sherehe ya kumuaga. Ziara ya Ujerumani ni ya 22 ya Baba Mtakatifu tangu alipochaguliwa kuliongoza kanisa Katoliki duniani mnamo mwaka 2005.

Wakati wa ziara hiyo, kiongozi huyo aliutembelea mji mkuu Berlin, Erfurt mashariki mwa Ujerumani na Freiburg, mji wenye idadi kubwa ya waumini wa kanisa Katoliki kusini magharibi mwa nchi.

Papa Benedict XVI aliwavutia maelfu ya waumini kwa ibada zilizofanyika kila mahali alikotembelea wakati wa ziara yake, ikiwa ni pamoja na misa ya mwisho iliyofanyika mapema jana ambayo ilihudhuriwa na watu takriban 100,000 katika uwanja wa ndege wa mjini Freiburg.

Katika kila kituo cha ziara yake Baba Mtakatifu alisisitiza umuhimu wa imani kama msingi wa demokrasia iliyo imara au kama chanzo cha nguvu iliyosaidia kupinga ukomunisti katika taifa la zamani la Ujerumani Mashariki.