1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baada ya shambulio: Jeshi la Ujerumani libaki Afghanisten?

Maja Dreyer21 Mei 2007

Baada ya kuuawa wanajeshi watatu wa Ujerumani katika shambulio dhidi ya jeshi hilo mjini Kundus, Afghanistan, juzi Jumamosi, kunafanyika mjadala mkali hapa nchini juu ya ujumbe wa kijeshi katika nchi hiyo. Wakati huo huo, wanajeshi wanne waliojeruhiwa katika shambulio hili wamerudishwa Ujerumani ili kutibiwa katika hospitali ya jeshi.

https://p.dw.com/p/CB42
Baada ya shambulio mjini Kundus
Baada ya shambulio mjini KundusPicha: AP

Leo asubuhi, wanajeshi wawili waliojeruhiwa kwenye shambulio la juzi la mjini Kundus, wameachiliwa kutoka hospitali, wengine wawili bado wako hospitalini. Lakini hawako hatarini tena, aliarifu msemaji wa hospitali. Maiti za wanajeshi watatu waliouawa zinatarajiwa kufikishwa Ujerumani Jumatano. Serikali ya Ujerumani iliwapa pole jamaa wa wahanga hao, lakini wakati huo huo ilidai kuwa kazi ya jeshi hilo nchini Afghanistan lazima iendelezwe.

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Franz Josef Jung, alisisitiza hasa mbinu ya jeshi hilo ya kuijenga upya Afghanistan: “Inabidi tuwashawishi watu watupende - hiyo ndiyo muhimu zaidi. Katika eneo la Kaskazini, tayari tumetekeleza miradi isiyopungua 650, ikiwa ni huduma za maji, kujenga barabara, hospitali na shule ze chekechea. Njia hiyo ndiyo inafaa na tutaiendeleza.”

Jumamosi asubuhi, mshambuliaji aliyejitoa muhanga alijilipua katikati ya barabara katika mtaa wa maduka mjini Kundus, Kaskazini mwa Afghanistan, akiwa ni kandoni mwa kundi la wanajeshi wa Ujerumani. Wanajeshi hawa walienda kwa miguu kununua friji kwa ajili ya kambi yao ya jeshi. Hiyo ni kulingana na mkakati wa jeshi la Ujerumani, yaani kuwasiliana kwa karibu na Waafghanistan na kuimarisha uchumi wa kienyeji. Pamoa na wanajeshi hao watatu wa Kijerumani, mshambuliaji aliwaua watu wanane walio raia wa kawaida.

Jeshi zima la Ujerumani nchini Afghanistan limesikitishwa sana na shambulio hili, alisema msemaji wa jeshi, Klaus Geier aliyepo Kabul: “Kila mmoja wetu aliathirika, wengi wameingiwa na hofu, kwa hiyo bila shaka pia hapa Kabul wanajeshi wote wanasikitishwa sana.”

Hata hivyo, wanajeshi wanataka kuendelea na kazi zao. Msemaji mwingine wa jeshi alisema: Ikiwa hatutaki kushindwa, lazima tubaki hapa.

Nchini Ujerumani lakini, wanasiasa wengi walidai kinyume chake au angalau kujadiliana upya juu ya kikosi cha jeshi na mbinu zake. Madai haya yametajwa hasa na vyama vya upinzani pamoja na Chama cha Social Democrats SPD. Mbunge Ottmar Schreiner wa chama cha SPD amenukuliwa na gazeti moja akisema haoni msingi wa amani katika jamii ya Afghanistan, na kwa sababu hiyo hakuna msingi wa kuendelea kuweko kikosi cha kijeshi huko. Chama cha Kijani kinataka juhudi zifanywe zaidi katika kujenga upya Afghanistan badala ya kuingilia kijeshi.

Rais Hamid Karsai wa Afghanistan alililaumu vikali shambulio hilo na kuongeza kusema kwamba maadui wa Afghanistan hawataweza kuzuia maendeleo ya nchi hiyo kwa kufanya vitendo vya woga kama hivyo.

Jana kumetokea shambulio lingine katika mkoa wa Paktia, Kusini Mashariki wa Afghanistan, ambalo limelilenga jeshi la Marekani. Waathirika lakini walikuwa raia wa kawaida tu, 14 kati wao wamefariki dunia. Wanamgambo wa Taliban wamedai kuhusika na shambulizi hilo na vile vile na lile la Kundus.