1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baada ya malumbano ya wiki kadhaa viongozi wakubaliana kuisaidia Ugiriki.

Abdu Said Mtullya26 Machi 2010

Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya wamefikia mapatano ya kuisaidia Ugiriki.

https://p.dw.com/p/MfFv
Waziri Mkuu wa Ugiriki George Papandreou akizungumza kwenye mkutano wa mjini Brussels wa viongozi wa Umoja wa Ulaya.Picha: AP

Wakuu wa nchi na viongozi wa serikali wa Umoja wa Ulaya leo wamemaliza mkutano wao mjini Brussels ambapo wamefikia mapatano juu ya kuisaidia Ugiriki.

Viongozi hao kutoka nchi 27 wamekubaliana juu ya mpango wa kuisaidia Ugiriki ikiwa nchi hiyo haitakuwa na uwezo wa kutafuta fedha kutokana na nguvu zake, ili kuweza kuyalipa madeni yake.

Marais na mawaziri wakuu wa nchi za Umoja wa Ulaya wamefikia mapatano yasiyokuwa na mithili juu ya kutenga mfuko wa fedha wa dharura kwa ajili ya kuisadia Ugiriki inayokabiliwa na madeni makubwa.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema ameridhishwa sana na matokeo ya mkutano huo na amesema kuwa matokeo hayo ni muhimu sana kwa sarafu ya Euro.

Bibi Merkel amesema nchi za Umoja wa Ulaya zimeonyesha uwezo wa kuchukua hatua linapohusu suala muhimu Kiongozi huyo wa Ujerumani amesema ni muhimu kwa nchi zote za Umoja wa Ulaya kwa sarafu ya Euro kuendelea kuwa imara.

Mapatano yaliyofikiwa yamefungua ukurasa mpya katika historia ya nchi za Umoja wa Ulaya zinazotumia sarafu ya Euro.Kwa mara ya kwanza Umoja wa Ulaya utaliruhusu shirika la fedha la Kimataiafa IMF kuwa na usemi katika masuala yanayohusu sarafu ya Euro.

Akisiitiza mafanikio ya mkutano wa mjini Brussels wa viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya rais wa kamisheni ya Umoja huo Jose Manuel Barroso ameeleza kuwa mkutano umefanikiwa sana siyo tu kwa sababu ya makubaliano ya kihistoria yaliyofikiwa juu ya kuisaidia Ugiriki na juu ya kudumisha uimara wa fedha katika ukanda wa sarafu ya Euro lakini pia kutokana na kuzizingatia changamoto za muda mrefu, ikiwa pamoja na suala la mabadiliko ya hali ya hewa na juu ya mkakati wa kudumisha ustawi na ajira.

Hata hivyo kuhusu Ugiriki Barroso ameyataka mabenki yaamue katika msingi wa ukweli na siyo katika msingi wa hoja za kubuni.

Ugiriki inatarajiwa kupata mkopo wa hadi Euro Bilioni 23.Theluthi 2 zitatolewa na nchi za kanda ya Euro na zilizobakia zitatolewa na shirika la fedha la kimataifa IMF.

Mwandishi/ Mtullya Abdu/DW/AFPE/ZA

Mhariri/Abdul-Rahman