1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baada ya kidole kukataliwa, sasa Rais Saleh atoa mkono

10 Machi 2011

Rais Ali Abdullah Saleh wa Yemen amependekeza kura ya maoni itakayoamua muundo mpya serikali, lakini wapinzani wake wanamuambia amechelewa sana na sasa hawakubali jengine zaidi ya rais huyo kuondoka madarakani tu.

https://p.dw.com/p/10X1g
Vidole vya muandamanaji wa Yemen
Vidole vya muandamanaji wa YemenPicha: picture alliance / dpa

Lau ahadi ya leo angeliitoa miezi miwili tu nyuma, ingelikuwa na maana kubwa na ingeliinusuru nchi yake na vifo vya watu 30, vilivyotokana na maandamano ya mwezi mmoja dhidi ya utawala wake.

Lakini ahadi ya leo ya Rais Ali Abdullah Saleh inachukuliwa na wapinzani kuwa ni kutapatapa na kupitisha muda tu, huku akihisabu siku zake madarakani.

Akizungumza na maelfu ya wafuasi wake kwenye uwanja wa michezo mjini Sanaa, kiongozi huyo mkongwe na sahibu mkubwa wa Marekani, ameahidi kura ya maoni juu ya katiba mpya, na pia kuvitaka vikosi vyake vihakikishe usalama wa waandamanaji, hata kama wanaupinga utawala wake.

"Napendekeza haya yafuatayo: kutaundwa kamati ya bunge na baraza la kuangalia mabadiliko ya katiba. Kutakuwa na serikali inayochaguliwa na watu wenyewe na ambayo itakaa madarakani kwa kipindi maalum tu." Alisema Rais Saleh.

Maandamano dhidi ya Rais Ali Abdullah Saleh wa Yemen
Maandamano dhidi ya Rais Ali Abdullah Saleh wa YemenPicha: picture alliance / dpa

Rais Saleh, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1978, amependekeza kuwa, Yemen iongozwe kwa mfumo wa kibunge, ambapo rais anakuwa alama tu ya taifa, huku nguvu zote zikiwa kwa waziri mkuu, ambaye anachaguliwa na bunge.

Lakini mapendekezo haya, hayakuwapa wapinzani kile hasa wanachokitaka, ambacho ni kiongozi huyo kuondoka madarakani.

Mara tu baada ya hotuba hiyo, iliyokuwa ikirushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni ya taifa, msemaji wa upinzani, Mohammad al-Sabri, aliliambia Shirika la Habari la AFP kuwa, ahadi hii ya mageuzi imekuja wakati imeshachelewa.

"Hatua za Rais zimekawia sana na zinaonesha utawala wake unapumulia upumzi wake wa mwisho madarakani." Amesema al-Sabri.

Maandamano dhidi ya Rais Ali Abdullah Saleh wa Yemen
Maandamano dhidi ya Rais Ali Abdullah Saleh wa YemenPicha: AP

Maelfu ya waandamanaji waliokusanyika uwanja wa Taghyeer, ulio karibu na chuo kikuu cha Sanaa, walipiga kelele za kumlaani Rais Saleh, wakimtaka aondoke mara moja, kama kweli anaipenda Yemen.

Karibuni madaktari 1,000 wakiwa na makoti yao nyeupe na makumi ya waandishi wa habari walijiunga na maandamano ya kukaa kitako chini ikiwa ni alama ya kumshinikiza Rais Saleh aondoke madarakani.

Yemen ni mshirika muhimu wa Marekani katika kile kinachoitwa vita vyake dhidi ya kundi la Al-Qaida katika Ghuba ya Uarabuni, ambalo linasemekana kuitumia nchi hiyo kupanga na kuendesha mashambulizi yake.

Hili linaifanya Marekani kutumia njia tafauti ya kuuzungumzia upinzani dhidi ya Rais Saleh, tafauti na inavyofanya kwa Muammar Gaddafi wa Libya.

Ambapo maandamano nchini Yemen yalianza wiki mbili kabla yale ya Libya, hakuna wakati ambapo Marekani imemtaka wazi Rais Saleh kuondoka madarakani kwa kuitikia matakwa ya wapinzani wake, ingawa imeshafanya hivyo mara kadhaa ndani ya wiki mbili hizi dhidi ya Gaddafi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE/ZPR
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman