1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaArmenia

Armenia waangazia kuwaondoa wapiganaji wao Karabakh

Lilian Mtono
22 Septemba 2023

Upande unaotaka kujitenga katika jimbo la Nagorno-Karabakh umesema mchana wa leo kwamba uko kwenye majadiliano kuhusiana na kuwaondoa wanajeshi wao kwenye eneo hilo linalozozaniwa kwa muda mrefu.

https://p.dw.com/p/4WhiN
Miongoni mwa waandamanaji wanaoishinikiza serikali ya Armenia kujibu operesheni ya kijeshi ya Azerbaijan katika jimbo la Nagorno-Karabakh
Miongoni mwa waandamanaji wanaoishinikiza serikali ya Armenia kujibu operesheni ya kijeshi ya Azerbaijan katika jimbo la Nagorno-KarabakhPicha: Karen Minasyan/AFP

Mazungumzo hayo yanafanyika baada ya Arzebaijan kuchukua tena udhibiti kufuatia operesheni kali ya kijeshi ya hivi karibuni. Hayo yanafanyika wakati Azerbaijan ikitangaza kupeleka misaada ya kiutu katika eneo hilo linalozozaniwa. 

Taarifa ya upande huo unaotaka kujitenga imesema mazungumzo na Azerbaijan bado yanaendelea kwa usimamizi wa walinda amani wa Urusi ili kuratibu mchakato wa kuwaondoa wanajeshi hao na kuhakikisha wanarejea makwao baada ya kuondoka kufuatia uvamizi wa kijeshi wa Azerbaijan.

Kiongozi wa kabila ya Armenia katika jimbo hilo lililojitenga la Nagorno-Karabakh amesema bado hakujafikiwa makubaliano na Azerbaijan juu ya dhamana ya usalama ama hata msamaha kwa wapiganaji, licha ya mshauri wa sera za kigeni wa rais wa Azerbaijan Hikmet Hajiyev kuliambia shirika la habari la Reuters kwamba, Baku inataka kuwasamehe wapiganaji wa Karabakh wa Armenia waliosalimisha silaha zao ingawa baadhi wameapa kuendeleza upinzani.

Waziri mkuu wa Armenia Niko Pashinyan amesema hali inazidi kuwa mbaya katika jimbo la Nagorno-Karabakh
Waziri mkuu wa Armenia Niko Pashinyan amesema hali inazidi kuwa mbaya katika jimbo la Nagorno-KarabakhPicha: Tigran Mehrabyan/PAN Photo/REUTERS

Hali inazidi kuwa mbaya.

Hali hii inazidi kuibua mashaka kuhusiana na mustakabali wa Karabakh pamoja na Waarmenia 120,000 wanaoishi kwenye jimbo hilo, wakati Azerbaijan ikitaka kuliunganisha jimbo hilo linalozozaniwa kwa muda mrefu, lakini Waarmenia wanasema wanahofia mateso huku wakiushutumu ulimwengu kwa kuwatelekeza.

Soma pia: Armenia na Azerbaijan zashambuliana kabla ya mkutano wa kutafuta amani

Kulingana na David Babayan, mshauri wa rais wa eneo lililojitangaza Jamhuri la Artsakh, Samvel Shahramanyan ameiambia Reuters kwamba bado hakujakuwa na matokeo yoyote ya maana hadi sasa, zaidi ya makubaliano ya kupeleka misaada ya kiutu kutokea Armenia kupitia ujia wa Lachin, hadi Karabakh.

Mapema, waziri mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan alionya juu ya hali inayozidi kuzorota katika jimbo la Nagorno-Karabakh wakati wa kikao cha baraza la mawaziri hii leo katika mji mkuu Yerevan.

Pashinyan amesema "Hakuna kitisho cha moja kwa moja dhidi ya maisha ya watu kwa sasa, lakini ieleweke kwamba hali inabadilika kila wakati. Siwezi kusema iko sawa kwa sasa, lakini haimaanishi kwamba kwenye baadhi ya maeneo na katika baadhi ya matukio hakuwezi kutokeo kitu."

Misaada ya kiutu inazidi kupelekwa katika jimbo la Nargono-Karabakh ambako kumeibuka mapigano yaliyobua mashaka makubwa ya kiusalama
Misaada ya kiutu inazidi kupelekwa katika jimbo la Nargono-Karabakh ambako kumeibuka mapigano yaliyobua mashaka makubwa ya kiusalamaPicha: Alexander Patrin/TASS/IMAGO

Misaada ya kiutu yaanza kupelekwa Nagorno-Karabakh.

Raia wameandamana kwa siku tatu mfululizo wakipinga namna serikali inavyoushughulikia mzozo uliopo na kumtaka Pashinyan kujiuzulu.

Arzebaijan, mchana huu imesema inapeleka misaada ya kiutu huko Karabakh na hasa kutokana na kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na dawa tangu mwezi Disemba mwaka uliopita, kutokana na vizuizi katika barabara inayounganisha jimbo hilo na Armenia. Azerbaijan imesema hatua hiyo itasaidia pakubwa kurejesha utulivu kwenye jimbo hilo lililo ndani ya Azerbaijan lakini likiwa chini ya udhibiti wa jeshi la watu wa kabila ya Armenia tangu mwaka 1994.

Azerbaijan inaungana na Umoja wa Ulaya ambaoo umesema utatoa yuro 500,000 kwa watu walioathirika na mzozo jimboni humo. Kamishna wa Ulaya anayeshughulikia mizozo Janez Lenarcic amesema wakati Umoja huo ukikaribisha makubaliano ya kusitisha mapigano, lakini unaziomba pande zinazohasimiana kuhakikisha mashirika ya misaada ya kiutu yanafika eneo la mzozo.

Kulingana na Halmashauri ya Ulaya, fedha hizo zitatumika kwa ajili ya mahitaji ya msingi, makazi na msaada wa kisaikolojia. Msaada huu mpya unatolewa pamoja na yuro milioni 1.7 zilizotengwa kwa ajili ya mzozo wa Nagorno-Karabakh mapema mwaka huu.