AU kujadili Burundi, Ugaidi na utata wa mihula | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.06.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

AU kujadili Burundi, Ugaidi na utata wa mihula

Viongozi wa mataifa ya Afrika wanakutana leo mjini Johannesburg, Afrika Kusini, katika mkutano wa kilele utakaoghubikwa na mzozo wa Burundi, na mgogoro wa uhamiaji barani humo.

Mwenyekiti wa AU, rais Robert Mugabe, na rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma

Mwenyekiti wa AU, rais Robert Mugabe, na rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma

Masuala mengine ambayo yanatarajiwa kupewa kipaumbele katika mkutano huo ni kitisho cha makundi yenye itikadi kali ya kiislamu, kama Boko Haram ambayo inaihangaisha Nigeria, mojawapo ya nchi muhimu katika Umoja wa Afrika.

Mtafiti katika Taasisi ya Afrika Kusini kuhusu Uhusiano wa Kimataifa, Tjiurimo Hengari, anasema miaka miwili ijayo itakuwa yenye changamoto kubwa kwa Umoja wa Afrika, hususan kutokana na wimbi la baadhi ya viongozi wa nchi za bara hilo kutaka kubadilisha katiba za nchi zao ili waweze kugombea muhula wa tatu au wa nne.

Hatua ya rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kuamua kugombea muhula wa tatu, ambao wapinzani wanasema inakwenda kinyume na katiba, imeitumbukiza nchi hiyo katika mzozo ambao tayari umewauwa watu 40 na kusababisha wengine takribani 100,000 kuikimbia nchi hiyo.

Masuala yenye utata

Rais Omar al-Bashir anayetafutwa na mahakama ya ICC

Rais Omar al-Bashir anayetafutwa na mahakama ya ICC

Hata hivyo, mkutano huo wa kilele ambao aghalabu huyakwepa masuala yenye utata, unaweza kughubikwa na sakata la rais wa Sudan Omar al-Bashir ambaye amewekewa waranti wa kukamatwa wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu,ICC anayetarajiwa kuwasili nchini humo. Rais huyo anatuhumiwa kutenda uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, na Afrika Kusini kama mwanachama wa mkataba wa Roma ulioiunda ICC, inao wajibu wa kumkamata.

Msemaji wa Umoja wa Afrika, AU, Molalet Tsedeke, amelithibitishia shirika la habari la AFP kuwa rais al-Bashir anatazamiwa kuhudhuria mkutano huo.

Marais wa kiafrika wamegawika kuhusu mkataba ulioianzisha mahakama ya ICC, na mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Januari mwaka huu aliwataka wenzake kuziondoa nchi zao katika mkataba huo.

Mugabe kung'ara jukwaani

Utata juu ya muhula wa tatu kwa rais Pierre Nkurunziza wa Burundi umeizamisha nchi hiyo katika ghasia

Utata juu ya muhula wa tatu kwa rais Pierre Nkurunziza wa Burundi umeizamisha nchi hiyo katika ghasia

Miongoni mwa viongozi watakaopanda jukwaa la mkutano huo leo Jumapili ni mwenyekiti wa AU rais Robert Mugabe,na mwenyeji, rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma. Rais mpya wa Nigeria Muhammadu Buhari vile vile anatarajiwa kushiriki katika mkutano, lakini marais wa nchi nyingine zenye uchumi mkubwa barani Afrika, Edouardo dos Santos wa Angola, na Abdel Fatah al-Sisi wa Misri hawatashiriki.

Mkutano huu wa kilele unafanyika nchini Afrika Kusini miezi miwili tu baada ya kuzuka kwa ghasia za chuki dhidi ya wageni, ambazo ziliwalenga wahamiaji kutoka nchi za kiafrika. Ghasia hizo zilizichukiza nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika, ambazo raia wake waliathiriwa zaidi. Raia saba wa nchi za kiafrika waliuawa katika ghasia hizo zilizoanzia katika mji wa Mashariki wa Durban.

Katika kile ambacho mchambuzi wa sera za Umoja wa Afrika Liesl Louw- Voudran nachokiita ''mwenendo usio wa kawaida'', suala la chuki ya wageni litajadiliwa katika kikao cha faragha, kabla ya ufunguzi rasmi wa mkutano leo hii.

Aidha, mkutano huo utalizungumzia tatizo la wahamiaji wa kiafrika na kutoka nchi za Mashariki ya Kati, ambao wanahatarisha maisha yao kwa kujaribu kuingia barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania. Watu wapatao 1,800 wameangamia katika safari za aina hiyo mwak huu pekee.

Mkutano huu wa kilele wa AU mjini Johannesburg umefanyika miezi mitano tu baada ya mwingine uliofanyika katika makao makuu ya umoja huo mjini Addis Ababa, Ethiopia Januari mwaka huu.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/ape

Mhariri: Sudi Mnette

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com