1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Asif Ali Zardari aapishwa kuwa rais wa Pakistan

Saumu Mwasimba9 Septemba 2008

Miongoni mwa masuala aliyoahidi ni pamoja na ushirikiano na Afghanistan kupambana na ugaidi

https://p.dw.com/p/FECF
Picha: AP

Kama mlivyosikia katika taarifa ya habari Asif Ali Zardari leo ameapishwa kuwa rais mpya wa Pakistan baada ya kuchaguliwa na wabunge mwishoni mwa wiki iliyopita.Zardari ambaye aliapishwa katika makaazi rasmi ya rais ameahidi kuitetea katiba na kuilinda nchi hiyo.

Asif Ali Zardari mume wa marehemu Benazir Bhutto aliyekuwa waziri mkuu wa Pakistan amekula kiapo cha kuitetea na kuilinda nchi yake kama rais wa taifa hilo katika sherehe iliyofanyika kwenye makaazi ya rais ambapo mgeni rasmi alikuwa ni rais wa Afghanistan Hamid Karzai.

Aidha mabalozi wa kigeni wanaofanyia kazi mjini Islamabad pia walihudhuria pamoja na maafisa wa ngazi za juu na wakuu wa kijeshi na familia ya bwana Zardari.Awali zilifanyika pia tambiko za kidini ikiwa ni pamoja na kuchinjwa mbuzi watatu weusi wakati Zardari alipoingia kwa mara ya kwanza hapo jana katika nyumba ya rais.

Akiwa amevalia mavazi ya jeshi la Majini na shati jeupe Zardari alikula kiapo na kuahidi kwamba kuanzia leo amekubali kutenda lolote kuilinda na kuitetea katiba ya jamhuri ya kiislamu ya Pakistan pamoja na wananchi wake.

Wakati akitia saini kiapo hicho ukumbi watu waliohudhuria sherehe hizo walipiga makofi huku wakimtaja mkewe rais mpya marehemu Benazir Bhutto aliyeuwawa kwa kupigwa risasi katika shambulio la bomu mnamo mwezi Desemba katika mkutano wa kampeini.

Zardari mwenye umri wa miaka 52 amechukua wadhifa huo wa rais baada ya rais Pervez Musharraf Kujiuzulu mwezi uliopita kuepuka kuondolewa kwa nguvu madarakani.

Hivi punde rais Karzai wa Aghanistan akiwa pamoja na mwenyeji wake Zardari katika mkutano na waandishi wa habari amempongeza rais huyo.Kwa upande mwingine Zardari amewashukuru wananchi wapakistan akisema sasa nchi hiyo ni ya demokrasia ya kweli.Halikadhalika amekiri kwamba nchi hiyo inakabiliwa na matatizo kadha wa kadha na akaahidi kushirikiana na Afghnaistan pamoja na nchi zingine za eneo hilo katika kuyatautua matatizo hayo ikiwa ni zaidi suala la kukabiliana na ugaidi.

Wadadisi wa mambo wanasema kuwa changamoto kubwa atakazokabiliwa nazo rais huyo ni kuudhibiti mfumko wa bei ambao sio tu unawaumiza zaidi watu maskini lakini pia unawaathiri watu wa tabaka la kati.

Changamoto nyingine ambayo inatajwa huenda ikapewa kipaumbele ni kuendelea kuweka mizani kati ya wapakistan wasiopendelea sera za Marekani na shinikizo za kuyaunga mkono mataifa ya magharibi katika vita dhidi ya ugaidi.

Hapo jana wanajeshi wa Marekani walivurumisha makombora katika eneo la waziristan kwenye chuo cha kiislamu kinachoendeshwa na kamanda wa kitaliban kutoka Afghanistan Jalaliddin Haqqani.

Kamanda huyo aliponea chupuchupu lakini watu 20 waliuwawa na wengine 25 wakajeruhiwa wengi wakiwa ni wanawake na watoto.Shambulio hilo limezusha hisia kali kwa wananchi wa Pakistan ambao wengi wamekuwa wakizidi kuitaka serikali yao ikomeshe uungaji mkono wa vita dhidi ya ugaidi na pia kuilazimisha Marekani kukomesha mashambulio yake katika eneo hilo.

►◄