1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ashton afanya ziara ya kihistoria Iran

9 Machi 2014

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, amesema hakuna uhakika ikiwa mataifa yenye nguvu duniani yatafikia makubaliano ya mwisho na Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia.

https://p.dw.com/p/1BMRR
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton katika mkutano na waandishi wa habari Tehran(09.03.2014).
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton katika mkutano na waandishi wa habari Tehran(09.03.2014).Picha: picture-alliance/dpa

Ashton ametowa kauli hiyo Jumapili (09.03.2014) mjini Tehran wakati akianza ziara ya kihistoria nchini Iran ambayo ni ya kwanza tokea ashike wadhifa huo hapo mwaka 2009 na ambayo inaonyesha kurekebishika kwa uhusiano kati ya mataifa ya magharibi na Iran.

Ziara hiyo inafanyika baada ya Iran kusaini makubaliano ya awali hapo Novemba 2013 na mataifa yenye nguvu duniani ambapo kwayo imekubali kudhibiti shughuli zake za nyuklia ili nchi hiyo ilegezewe vikwazo ilivyowekewa.

Makubaliano hayo yaliweza kufanikiwa kutokana na kuchaguliwa kwa Rais Hassan Rouhani katika uchaguzi wa mwaka jana ambaye anaonekana kuwa ni mtu wa msimamo wa wastani na ambaye anasikilizwa na Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo, Ayatollah Ali Khamenei.

Makubaliano ya mwisho ni magumu

Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif mjini Tehran, Ashton amekaririwa akisema "Makubaliano hayo ya muda ni muhimu sana lakini sio muhimu kama makubaliano ya mwisho ambayo ni magumu na yenye changamoto na ambayo hakuna uhakika kwamba tutafanikiwa."

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton na waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif katika mkutano na waandishi wa habari Tehran(09.03.2014).
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton na waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif katika mkutano na waandishi wa habari Tehran(09.03.2014).Picha: picture-alliance/dpa

Ashton amesema ni muhimu sana kwa kazi hiyo kuendelezwa na Waziri Zarif na timu yake kwa kuungwa mkono na wananchi wa Iran na kwa kazi yake yeye kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa ambapo dhamira iwe katika kujaribu kufanikisha makubaliano hayo.

Kwa upande wake, Waziri Zarif amesema makubaliano ya mwisho kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yanaweza kufikiwa miezi michache ijayo na kwamba iwapo upande wa pili utakuwa na motisha kama ile ya Iran, suala la mzozo huo wa nyuklia linaweza kutatuliwa katika kipindi cha miezi minne ijayo.

Zarif amesema Iran imeazimia kufikia makubaliano hayo na imeonyesha nia njema na nia ya kisiasa na hivyo kutimiza wajibu wao "lililobaki ni kwa upande wa pili kutimiza wajibu wao." Ameongeza kusema makubaliano hayo yatahitaji kuheshimu haki za wananchi wa Iran na kuzingatia maslahi ya taifa hilo bila ya ubabaishaji.

Rouhani ashinikizwa

Katika ziara yake hiyo, Ashton anatazamiwa kukutana Rais Hassan Rouhani ambaye anashinikizwa kutoa tamko la kutaka vikwazo vya mafuta na vyenginevyo vyenye kuiathiri nchi hiyo viondolewe haraka iwezekanavyo ili kuufufuwa uchumi.

Rais Hassan Rouhani wa Iran.
Rais Hassan Rouhani wa Iran.Picha: Irna

Ziara hiyo ya Ashton imeelezewa na mwanadiplomasia mmoja wa Ulaya mjini Tehran kuwa ni "ishara ya nia njema kutoka Umoja wa Ulaya."

Lakini Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameikosoa ziara hiyo, akisema angelipenda kumuuliza Ashton iwapo aliwauliza wenyeji wake wa Iran kuhusu kupelekewa silaha kwa makundi ya kigaidi na iwapo hakuwauliza kwa nini hakufanya hivyo? Netanyahu alikuwa akikusudia meli iliyokuwa imenaswa na jeshi la Isael ikidaiwa kusafirisha silaha kutoka Iran kwenda Gaza.

Ajenda ya haki za binaadamu

Suala la haki za binaadamu pia limo kwenye ajenda ya Ashton licha ya uwezekano wa kuwatibuwa wahafidhina wa misimamo mikali nchini humo.

Wakili wa haki za binaadamu nchini Iran Nasrin Sotudeh.
Wakili wa haki za binaadamu nchini Iran Nasrin Sotudeh.Picha: picture-alliance/dpa

Kundi la bunge la wajumbe wanane wa Umoja wa Ulaya lilitembelea Iran mwezi wa Disemba 2013 na kukutana na wakili wa haki za binaadamu Nasrin Sotoudeh na mtengenezaji wa filamu Jafar Panahi na kuzusha shutuma kutoka kwa wahafidhina hao.

Mbunge mmoja wa Iran, Kazem Jalali, aliuita mkutano huo ni sawa na uingiliaji kati wa masuala ya ndani ya Iran. Sotoudeh na wafungwa wengine kadhaa wa kisiasa waliachiliwa kutoka gerezani mwezi wa Septemba mwaka jana kama sehemu ya sera ya Rouhani ya kujijengea haiba yake.

Mataifa sita yenye nguvu duniani - matano yakiwa wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa: Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi na China - pamoja na Ujerumani ambayo sio mwanachama wa kudumu, wanataraji kufikia makubaliano ya kudumu na Iran ifikapo tarehe 20 Julai baada ya kumalizika kwa muda wa makubaliano ya awali.

Mazungumzo rasmi kati ya Iran na mataifa hayo yamepangwa kufanyika tarehe 17 hadi 20 Machi, mjini Vienna, Austria.

Ziara hiyo ya Ashton nchini Iran ni ya kwanza kufanywa na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya tokea ile iliyofanywa na mtangulizi wake Javier Solana hapo mwaka 2008.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef