1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Asasi za kiraia zalia na hitilafu uchaguzi DRC

Zainab Aziz
30 Desemba 2018

Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wamepiga kura ya kumchagua rais mpya wa nchi yao huku asasi za kiraia zikilalamika juu ya hitilafu kadhaa zilizojitokeza pia kukiwa na wasiwasi wa kuzuka ghasia.

https://p.dw.com/p/3Amp5
Wahlen im Kongo
Picha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Msemaji wa asasi ya kiraia ya Symotel Luc Lutala amedai kwamba walichoshuhudia kimevuka hofu walizokuwa nazo. Msemaji huyo Lutala ameeleza kuwa vituo kadhaa vya kupigia kura vilihamishwa mnamo dakika za mwisho  kwa lengo la kuwakanganya wapiga kura. Kulingana na taarifa zilizopokewa na asasi hiyo ya kiraia-Symotel, kutoka kwenye kila  jimbo mashine za kupigia kura wakati mwingine hazikufanya kazi. Asasi hiyo ya kiraia  ina waangalizi 19,000 nchini Kongo  kote. Kundi hilo la kiraia pia limesema katika kadhia nyingine kadhaa,  madaftari ya kupigia kura yalitoweka. Hata hivyo idadi kamili haijulikani.

Uchaguzi huo wa rais ni wa kwanza katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo utakaotoa fursa ya kuleta  mabadiliko ya uongozi kwa njia ya  amani na kidemokrasia tangu nchi hiyo  ijipatie uhuru wake mnamo  mwaka 1960  ikiwa rais aliyeko madarakani Joseph Kabila ataachia ngazi.

Wasiwasi juu ya kuzuka ghasia ulitanda baada ya kupitishwa uamuzi wa kutowashirikisha watu wapatao milioni moja katika kupiga kura kutokana na mripuko wa maradhi ya Ebola mashariki mwa nchi hiyo.  Uamuzi huo umeshutumiwa kutoka pande mbalimbali kwa kuwa unahujumu uhalali wa uchaguzi.

Mgombea wa chama tawala Ramazan Shadary
Mgombea wa chama tawala Ramazan ShadaryPicha: DW/S. Schlindwein

Katika mji wa Beni, ambao ni miongoni mwa miji mitatu ya mashariki ambako uchaguzi umeahirishwa hadi mwezi wa Machi, mamia ya vijana walijipigia kura ya mfano kuashiria upinzani dhidi ya uamuzi wa kuchelewesha zoezi la kupiga kura. Vijana hao waliimba huku wakitamka kuwa kupiga kura ni haki yao na  kwamba hakuna atakaeweza kuwazuia.

Wananchi katika miji ya Beni na Butembo hawatapiga kura kwenye uchaguzi wa tarehe 30 Desemba lakini licha ya kukatazwa kupiga kura, watu wapatao 10,000 walionekana wamejipanga katika  foleni wakisubiri kupiga kura katika sehemu kadhaa za mji wa Beni.

Kwa mujibu wa taarifa mshindi wa uchaguzi huo wa rais atatangazwa na kuapishwa kabla ya wananchi katika miji hiyo kupiga kura. Mkaazi mmoja wa Beni Jacob Salumu amesema kura zao walizopiga kama mfano pia zinapaswa kutiwa katika hesabu sawa na zile za wananchi wengine. Salumu amesema ameenda kupiga kura kwa sababu hiyo ni haki yake. Mwananchi huyo amesema yeye na wenzake hawana maradhi ya Ebola.

Katika kadhia nyingine mgombea wa upinzani Martin Fayulu alipiga kura mjini Kinshasha kwenye kituo  ambapo, hapo awali rais anayeondoka madarakani Joseph Kabila na mgombea wa chama tawala Emmanuel Shadary walipiga kura zao. 

Mgombea wa upinzani Martin Fayulu
Mgombea wa upinzani Martin FayuluPicha: Getty Images/AFP/T. Charlier

Fayulu amesema uchaguzi huu ndiyo mwisho wa Kabila. Alisema wakati alipopiga kura kwamba huu ndio  mwisho wa dhiki kwa watu wa Kongo. Amesema Kongo haitakuwa tena kichekesho duniani na kwamba  matokeo yataonyesha kile ambacho watu wa Jamhuri ya Kidemkorasia ya Kongo wanakitaka.

Kwa upande wake rais Kabila, ambaye amekuwamo madarakani kwa muda wa miaka 18 alitoa wito kwa  wafuasi wao wa kujitokeza, licha ya mvua kubwa, ili kuwapigia kura wagombea wao. Mgombea wa chama  tawala, Shadary ametoa wito wa kudumisha amani na utulivu na ameelezea uhakika wa kushinda kwa sababu amesema watu wa Kongo wana imani nae.

Tume ya uchaguzi imejaribu kuwahakikishia wapinzani kwamba nakala za vikaratasi vya kura kutoka  kwenye mashine zitazingatiwa katika hesabu. Wakati huohuo Papa Francis amewaombea wahanga  wa ukatili na wale wanaougua maradhi ya Ebola na pia ametoa wito wa amani kwa watu wa Kongo.

Mwandishi:Zainab Aziz/AP/RTRE/AFPE

Mhariri: Jacob Safari