1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Annalena Baerbock mgombea ukansela wa chama cha Kijani

Iddi Ssessanga
19 Aprili 2021

Chama cha watetezi wa mazingira cha Ujerumani, Die Grüne, kimemteua Annalena Baerbock, mmoja wa mwenyekiti mwenza kuwa mgombea wake wa nafasi ya Kansela katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Septemba.

https://p.dw.com/p/3sF1L
Deutschland Kanzlerkandidat der GRÜNEN
Picha: dpa/picture alliance

Chama hicho kimepata umaarufu zaidi katika uchunguzi wa maoni ya wapigakura katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, na hii ndiyo mara ya kwanza kwake kuteua mgombea mmoja wa nafasi ya kansela, wakati ambapo Angela Merkel anaachia ngazi baada ya kuongoza kwa zaidi ya miaka 15.

Annalena Baerbock alivutia nadhari wakati wa mkutano mkuu wa chama mapema 2018. Akiwa amevalia koti lake la rangi nyeusi, mwanasiasa asiejulikana kutoka jimbo la Brandenburg, alijotokeza mbele na kuuahidi mkutano.

Wajumbe wa chama cha Kijani walimchagua kuwa mmoja wa viongozi wenza wa chama hicho. Hatua hiyo ilikuwa, na bado ni ya kihistoria. Kimsingi, chama hicho cha watetezi wa mazingira kilikuwa na nyota moja tu: Robert Habeck alikuwa anazungumziwa kisirisiri kama mtu anaweza kuwania ukansela.

Deutschland Grünen-Vorstand macht Vorschlag für Kanzlerkandidatur | Annalena Baerbock
Annalena Baerbock akitambulishwa na mwenyekiti mwenza wa chama cha Die Grüne Robert Habeck, kuwa mteule wa nafasi ya kansela katika uchaguzi 2021.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Na tangu kupanda kwake katika nafasi ya mwenyekiti mwenza wa chama, Baerbock hajarudi tena nyuma. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 40 ameunoa wasifu wake wa kisiasa kama mtaalamu wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Na haoni aibu kuzungumzia masuala tete ya kigeni.

Na pia amezungumzia vitisho vinavyosababishwa na itikadi kali ya mrengo wa kulia na chuki dhidi ya wageni. Hivyo, wakati mkutano wa chama ulipoitishwa tena majira ya baridi mwaka 2019, Baerbock aliungwa mkono na asilimia 97 ya wajumbe, na kumshinda Habeck, aliyepata asilimia 90.

Soma pia: Je chama cha Kijani Ujerumani ni chama kipya cha umma?

Annalena Baerbock  anachukuliwa kama mtu mwenye maamuzi, shujaa, mwenye malengo makuu na anaejiamini. Katika mahojiano ya pamoja na Habeck walioyatoa kwa jarida la kila wiki la Ujerumani la Der Spiegel mwishoni mwa mwezi Machi, alinukuliwa akisema kwamba iwapo Habeck na siyo yeye atateuliwa kupeperusha bendera ya chama chao kuwania nafasi hiyo ya juu kabisaa nchini Ujerumani, ingekuwa kwa kweli pigo dogo moyoni.

Deutschland Bundestag Baerbock Haushaltsdebatte
Annalena Baerbock akichangia mjadala katika bunge la Ujerumani Bundestag, huku kansema Angela Merkel akifutialia. Picha: dpa/picture alliance

Baerbock aliezaliwa mwaka 1980 katika mji mdogo wa Patternsen jimboni Lower Saxony, alikuwa mwanariadha, akishika nafasi ya tatu pia katika mashindano ya kitaifa ya ubingwa wa sarakasi. Alikuwa na umri wa miaka 16 tui wakati alipohamia Marekani kwa mwaka mmoja.

Baadae alisomea sheria mjini Hannover, kabla ya kujiunga na shule ya uchumi ya London, ambako alijikita katika sheria ya kimataifa. Kutokana na hilo, Baerbock anaweza kuzungumza lugha ya Kiingereza kwa ufasaha, jambo ambalo mpaka wakati huu halichukuliwi kimzaha miongoni mwa wanasiasa wa Ujerumani.

Mchakato wa uteuzi ndani ya chama cha die Grüne, umekuwa kinyume kabisaa na mapambano ya kuwania madaraka ndani ya muungano wa vyama vya kansela Angela Merkel vya CDU na CSU, ambayo yamendelea kwa wiki ya pili sasa. Uchaguzi wa Septemba 26 hautabiriki, kwa sehemu, kutokana na ukweli kwamba kansela wa sasa hagombei tena. Merkel aliahidi mwaka 2018 kwamba hangetafuta muhula wa tano wa miaka minne.

Uchunguzi wa karibuni wa maoni ya wapigakura unaonesha kuwa chama cha Kijani kikiwa katika nafasi ya pili baada ya muungano wa wahafidhina wa Merkel, na mbele ya chama cha jadi cha kisoshalisti cha Social Democratic SPD. Ugombea wa Baerbock utahitaji kuidhinishwa na mkutano mkuu wa chama mnano mwezi Juni.