1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ANKARA : Uturuki yakasirishwa na azimio juu ya Waarmenia

11 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Gh

Uturuki leo imeonya kwamba uhusiano na Marekani mshirika wake wa Umoja wa Kujihami wa Mataifa ya Magharibi NATO utaathiriwa na kuidhinishwa na kamati ya bunge la Marekani kwa azimio lenye kuyaita mauaji yaliofanywa na Waturuki kwa takriban Waarmenia milioni moja na nusu wakati wa Vita Vikuu vya kwanza vya Dunia hapo mwaka 1915 kuwa ni mauaji ya kimbari.

Uturuki daima imekuwa ikikanusha kwamba kulitokea mauaji ya kimbari na inaona maelezo hayo kuwa ni tusi. Rais George W. Bush wa Marekani pia alionya na mapema kwamba muswada huo unaweza kuharibu uhusiano na Uturuki ambayo ni mshirika wake kwenye Umoja wa Kujihami wa Mataifa ya Magharibi NATO na muungaji mkono muhimu wa Marekani katika vita dhidi ya ugaidi.

Akitetea azimio hilo mbunge wa chama cha Demokrat nchini Marekani Brad Sherman anasema hawawezi kutowa kanusho la mauaji ya kimbari kama mojawapo ya marupurupu ya urafiki na Marekani.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice leo anatazamiwa kuzungumza na waziri mwenzake wa Uturuki katika juhudi za kutululiza hali hiyo.

Hayo yanakuja wakati Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayip Erdogan akijiandaa kuliomba bunge ambalo linadhibitiwa na chama chake kuidhinisha kutuma jeshi lake kaskazini mwa Iraq kupambana na waasi wa Kikurdi wa Uturuki wanaolitumia eneo hilo kama ngome.

Waasi hao wamewauwa wanajeshi 15 wa Uturuki tokea Jumapili iliopita.