Angela Merkel ziarani Israel | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.02.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Angela Merkel ziarani Israel

Ziara ya Merkel itakuwa ya siku mbili na inalenga kuboresha uhusiano baina ya Ujerumani na Israel na pia kujadili kuhusu amani kati ya Israel na Palestina. Merkel anasindikizwa na ujumbe wa mawaziri wake 16.

Msemaji wa Kansela Merkel ameiita ziara hii ya kihistoria. Haijawahi kutokea kuwa Merkel amesafiri na karibu baraza zima la mawaziri kwenda Israel. Mada muhimu zitakazojadiliwa ni namna ya kuboresha ushirikiano katika masuala ya utafiti wa kisayansi baina ya nchi hizo mbili. Pamoja na hayo, Merkel atatumia nafasi hii kuandaa maadhimisho ya miaka hamsini tangu kuanzishwa kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Ujerumani na Israel. Merkel atakutana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na vilevile kufanya mazungumzo na rais Shimon Peres wa nchi hiyo. Peres atampa Merkel medali ya ubora ambayo ni tuzo kubwa zaidi inayotolewa na rais wa Israel.

Maeneo ya walowezi tatizo sugu

Wakati wanasiasa hao wanajaribu kuonyesha picha ya uhusiano mzuri, wachambuzi wa mambo wanaeleza kwamba hali si shwari. Gazeti la Haaretz la Israel hivi karibuni liliandika kuwa uhusiano kati ya Ujerumani na Israel haujawahi kuwa mbaya kama ulivyo sasa. Gazeti hilo limetoa kauli hiyo likizingatia uchambuzi uliochapishwa katika jarida la Der Spiegel la hapa Ujerumani, uchambuzi unaolelezea tofauti za mawazo kati ya Netanyahu na Merkel.

Maeneo ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi

Maeneo ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi

"Inasemekeana kwamba ilifikia mahali wanasiasa hao wakakaripiana kwenye simu. Ni kweli kwamba kuna tofauti katika serikali hizo. Ujerumani inapingana na suala la Israeli kujenga makaazi ya walowezi kwenye ardhi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi na kusema kwamba hilo ni jambo linalozuia jitihada za kuleta amani.

Tunahitaji suluhu ya mataifa mawili ambapo patakuwa na taifa la kiyahudi la Waisraeli pamoja na taifa kwa ajili ya Wapalestina," amesema Merkel. "Ninaamini kwamba sisi kama marafiki tunaweza kusaidia na tunapaswa kumuunga mkono waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry pamoja na wengine wanaojadili kuhusu amani mashariki ya kati."

Umoja wa Ulaya watoa masharti

Hata hivyo Israel inashikilia mpango wake wa kujenga maakazi ya walowezi mashariki mwa Jerusalem na katika Ukingo wa Magharibi mwa mto Jordan. Suala hilo limeleta pia msukosuko katika uhusiano wa Israel na Umoja wa Ulaya. Mwaka uliyopita, Umoja huo ulitoa mabilioni ya Euro kwa ajili ya kufadhili shughuli za utafiti Israel, kwa masharti kwamba fedha hizo haziruhusiwi kutumika katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa na W-aisraeli.

Kwa Ujerumani ni muhimu sana kuwa na uhusiano mzuri na Waisraeli kwani mamillioni ya wayahudi waliuliwa Ujerumani katika utawala wa Kinazi.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com