1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ANC yasherehekea ushindi mkubwa.

24 Aprili 2009

Kinara wa chama tawala cha Africa National Congress, ANC nchini Afrika Kusini, Jacob Zuma, jana aliwaongoza wafuasi wa chama hicho kusherehekea ushindi wao mkubwa.

https://p.dw.com/p/HdCQ
Jacob Zuma, kinara wa ANC akihutubia wafuasi wa chama hicho, mjini JohannesBurg:Picha: AP


Thuluthi mbili ya kura tayari zimehesabiwa na kama ilivyobashiriwa ANC haikutingishwa na upinzani, na sasa inaelekea kitapata thuluthi mbili ya viti bungeni.

ANC Anhänger in Pretoria
Wafuasi wa ANC wabeba mabango ya chama hicho.Picha: picture-alliance/ dpa

Huku matokeo yakiwa bado yanaendelea kuingia siku mbili baada ya raia nchini Afrika Kusini kufanya maamuzi- chama tawala cha ANC kinaongoza kwa 67 asilimia, hii inaashiria ANC kitaendelea kudhibiti wingi wake wa thuluthi mbili bungeni- na kutupilia mbali ule wasiwasi kuwa upinzani utakitingisa chama hicho kinachoongozwa na Jacob Zuma.


Chama rasmi cha upinzani Demokratic Alliance kimefanikiwa kupata aslia mia 16 ya kura. Chama cha Congress of the People au COPE, kinachoongozwa na wanachama waliojitoa kutoka ANC baada ya kujiuzulu kwa rais wa zamani Thabo Mbeki hakikupiga hatua kama ilivyotarajiwa.


Ilikuwa imebashiriwa huenda COPE kikakipa ANC kibarua katika miji mikuu kama vile Johannesburg, Cape Town, na Durban. Lakini COPE kimeweza kupata aslia mia 8 ya kura hadi kufikia sasa.


Südafrika Wahl Parteien ANC Jacob Zuma
Jacob Zuma, kuapishwa kama rais wa Afrika Kusini, mwezi ujao.Picha: AP

Na ndio maana Zuma hakupoteza wakati- wa kusherehekea. Katika mkutano mkubwa mjini Johannesburg Zuma aliwaongoza wafuasi wa ANC katika shangwe za kusherehekea ushindi wao katika makao makuu ya chama cha hicho.


Hata hivyo ANC imepoteza udhibiti wake katika mkoa wa CAPE magharibi. Chama rasmi cha upinzani Demokratic Alliance kinachoongozwa na Hellen Zille kiko imara mkoani humo.


Zuma anayetarajiwa kuapishwa kama rais mwezi ujao- hatopata muda wa kupumzika kwani Afrika Kusini- inakumbwa na matatizo mengi ikiwepo msukosuko wa masoko kutokana na mgogoro wa kiuchumi duniani.


Lakini kubwa zaidi- Zuma itabidi apambane na vipi atakavyoimarisha hali ya maisha ya raia wengi nchini Afrika Kusini. Ni kauli mbiu hii ya kuwa walio maskini wamesahaulika ndio iliyotumiwa na upinzani kujiimarisha katika uchaguzi huu.


Kama kiongozi wa chama kikubwa, atakapokuwa rais wa nne wa Afrika kusini, Zuma atakuwa anafuata nyayo za watangulizi wake, Mzee Nelson Mandela, Thabo Mbeki na Kgalema Motlanthe. Motlanthe amekuwa rais kwa miezi saba tu tangu kujiuzulu kwa Mbeki.


Mwandishi: Munira Muhammad/Reuters

Mhariri: Saumu Mwasimba