ANC yamshinikiza Jacob Zuma ajiuzulu | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.02.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

ANC yamshinikiza Jacob Zuma ajiuzulu

Chama tawala nchini Afrika Kusini bado kinaendelea kumshinikiza Rais Jacob Zuma aachie madaraka kwa hiyari yake, baada ya kiongozi huyo anayekabiliwa na kashia kadhaa za kifisadi kukataa kujiuzulu.

Viongozi wa chama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC, katika kikao chao kilichomalizika usiku wa kuamkia leo wamefikia makubaliano kuwa Rais Zuma lazima ang'oke madarakani.

Halmashauri Kuu ya ANC yenye wajumbe 107 ilikutana kwa masaa 13 katika hoteli moja nje ya mji wa Pretoria na kupitisha uamuzi huo wa kumtaka Zuma aondoke madarakani.

Vyombo vya habari vingine vimeripoti kuwa chama cha ANC kitamuandikia Zuma kikimuamuru kujiuzulu kama rais wa nchi hiyo baada ya ombi lake la kutaka kuendelea kusalia madarakani kwa miezi kadhaa kukataliwa.

Shirika la Utangazaji la nchi hiyo, SABC, limesema chama cha ANC kimempatia Zuma masaa 48 kuwa tayari amewasilisha barua yake ya kujiuzulu. Hata hivyo, maafisa wa chama hicho hawakupatikana kuthibitisha taarifa hizo, ingawa chama hicho kimeitisha mkutano na waandishi wa habari baadaye hii leo katika makao makuu ya chama hicho mjini Johannesburg.

Chama cha ANC kinaweza kumlazimisha Zuma ajiuzulu lakini mamlaka hayo yanaishia katika ngazi ya chama tu na habanwi na katiba ya nchi hiyo  kulazimika kujiuzulu.

 

Zuma huenda akaondolewa kupitia Bunge

Südafrika ANC Parteitag Ramaphosa (picture-alliance/AP Photo/T. Hadebe)

Mwenyekiti wa chama cha ANC, Cyril Ramaphosa

Iwapo atakataaa kujiuzulu, basi huenda akaondolewa madarakani kupitia bunge kwa kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye. Hoja ya upinzani dhidi ya Zuma ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye inayoungwa mkono imepangwa kufanyika Februari 22 lakini wafadhili wa hoja hiyo wanataka hoja hiyo irejeshwe wiki hii.

Wakati shinikizo la kumuondoa Zuma madarakani likizidi kupamba moto, mwenyekiti wa ANC, Cyril Ramaphosa,  inaripotiwa aliondoka katika kikao cha jana usiku na kwenda kuzungumza ana kwa ana na Rais Zuma katika makao yake rasmi mjini Pretoria lakini hata hivyo msafara wa magari wa Ramaphosa ulionekana ukirejea katika mkutano huo jana usiku na saa tatu baadaye mkutano huo ulimazika.

Cyril Ramaphosa anayetarajiwa kushika madaraka ya urais pindi Zuma atakapoaoondoka madarakani amekuwa  akifanya mazungumzo na rais Jacob Zuma  tangu alipokataa ombi la viongozi wa chama hicho la kumtaka kujiuzulu zaidi ya wiki moja iliypita.

Mkwamo huuu wa kisiasa nchini Afrika Kusini umeiingiza nchi hiyo katika mashaka makubwa kiutawala  na kushindwa kujua nani hasa kwa sasa anaongoza nchi hiyo mnamo wakati pia matukio muhimu ya kitaifa yakifutwa ikiwemo hotuba ya kila mwaka ya kitaifa katiba bunge la nchi hiyo iliyokuwa itolewe Alhamisi iliyopita.

Akihutubia mkutano wa hadhara wa chama cha ANC  jumapili mjini Capetown, Cyril Ramaphosa mwenye umri wa miaka 65, huku akishangiliwa aliwaeleza wanachama wa ANC kuwa yeye na viongozi wenzake wanatambua juu ya shauku walio nayo ya kutaka suala hilo limalizike haraka na kuwaahidi  kuwa halimashauri kuu ya chama  haitawaangusha na itafanya kwa ufasaha jambo hilo.

Zuma ambaye alichukua madaraka mwaka 2009 na  akiwa katika muhula wake wa pili na wa mwisho ameomba apewe ulinzi kwa familia yake pamoja , kulipiwa gharama za kisheria  na kuruhusiwa kukaa madarakani miezi kadhaa kama sharti la kumtaka aondoke madarakani. Hiyo ni kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Afrika Kusini.

Mwandishi: Isaac Gamba/ape/afpe

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com