1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amri ya kutotembea usiku yaendelea Baltimore

1 Mei 2015

Polisi mjini Baltimore waliendeleza marufuku yao ya kutotoka nje nyakati za usiku kwa siku ya tatu mfululizo huku maandamano mapya yakiibuka kwenye miji mingine ya nchini Marekani juu ya kifo cha kijana mweusi.

https://p.dw.com/p/1FIg8
Baltimore / Ausgangssperre / Polizei
Picha: Reuters

Usiku wa Alhamisi ulipita kwa utulivu kiasi ingawa polisi ilikabiliana kwa muda mfupi na kundi la waandamanaji mjini Baltimore, kiini cha machafuko ya karibuni kabisa yanayohusishwa na hasira juu ya namna vyombo vya usalama vinavyowatendea Wamarekani weusi, hasa vijana wa kiume.

Freddie Gray alipata majeraha akiwa mikononi mwa polisi, na taarifa zaidi juu ya namna kijana huyo alivyopata majeraha hayo zimeanza kuzuka na inahofiwa kuwa zitasababisha machafuko makubwa zaidi.

Watu wapatao 600 waliandamana kwenye mji huo wenye wakaazi 620,000 na ulio umbali wa mwendo wa saa moja kutoka mji mkuu wa Marekani, Washington, na ambao una historia ya machafuko kwa miongo kadhaa sasa.

Waandamanaji wakiwa wamebeba picha ya kijana aliefariki mikononi mwa Polisi Freddie Gray.
Waandamanaji wakiwa wamebeba picha ya kijana aliefariki mikononi mwa Polisi Freddie Gray.Picha: Getty Images/K. Betancur

Wataka marehemu atendewe haki

Maandamano yalishuhudiwa pia mjini Philadelphia, ambako waandamanaji walitoa wito wa kutendwa haki kwa kijana Freddie Gray. Mitaa ya New York, Washington na Boston yote imekuwa ikishuhudia maandamano tangu majuzi, na polisi inasema inawashikilia watu zaidi ya 140 ikiwahusisha na ghasia zinazoambatana na maandamano hayo.

Freddie Gray mwenye umri wa miaka 25 alifariki dunia wiki mbili zilizopita, lakini ghasia zilianza siku kadhaa baada ya kifo chake kuthibitishwa kuwa kilitokana na kuharibika kwa asilimia 80 ya uti wake wa mgongo baada ya kujeruhiwa akiwa mikononi mwa polisi.

Mazingira ya kukamatwa kwake hapo tarehe 12 Aprili na namna alivyopata majeraha hayo yaliyopelekea kifo chake wiki moja baadaye, bado yanazusha wasiwasi. Vyanzo mbalimbali vinasema uchunguzi wa kitabibu umegundua kijana huyo alivunjika shingo na uti wa mgongo, baada ya kutupwa kwenye karandinga la polisi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jeraha alilolipata kijana huyo kichwani linafanana na bolti iliyoko nyuma ya karandinga hilo, ingawa hadi sasa haifahamiki ni kitu gani kilichomsukuma. Polisi inasema gari hilo liliwahi kusimama mara moja njiani baada ya kumchukua Gray kabla ya kumfikisha kituo cha polisi.

Polisi ikimtia nguvuni moja wa washiriki wa maandamano ya mshikamano mjini Baltimore siku ya Alhamisi.
Polisi ikimtia nguvuni moja wa washiriki wa maandamano ya mshikamano mjini Baltimore siku ya Alhamisi.Picha: Getty Images/K. Betancur

Taarifa mpya yasubiriwa kwa hamu

Naibu Kamishna wa Polisi wa Baltimore, Kevin Davis, hakufafanua zaidi juu ya umuhimu wa ushahidi huu mpya, huku wakili wa familia ya Gray, Mary Koch, akisema hawezi kuuthibitisha kwa sasa. Kamishna wa Polisi wa Baltimore, Anthony Batts, na familia ya Gray wametoa wito kwa watu kutulia kungojea taarifa kamili, ambayo walisema wanatazamia haitasambaza sumu zaidi kwa kile ambacho tayari kinatokea.

Matukio ya polisi nchini Marekani kutumia nguvu za ziada dhidi ya raia wenye asili za Kiafrika ama Kilatino yanazidi kuripotiwa kila uchao, na kwa siku za karibuni kuripotiwa kwa matukio hayo kumekuwa kukifuatiwa na maandamano na ghasia katika kiwango ambacho hakikuwahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa sasa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Saumu Yussuf