1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty yaituhumu UAE kwa kuwapa silaha waasi wa Yemen

Amina Mjahid
6 Februari 2019

Shirika la Amnesty International limeishutumu Umoja wa Falme za kiarabu kuyapa silaha zinazotolewa na mataifa ya Magharibi na mataifa mengine, makundi ya wapiganaji yanayoshutumiwa kufanya uhalifu wa kivita Yemen.

https://p.dw.com/p/3Cpbr
Jemen Houthi-Kämpfer unterstützen Friedensgespräche
Picha: picture alliance/AP Photo/H. Mohammed

Umoja wa Falme za kiarabu na Saudi Arabia wanaoongoza muungano wa kijeshi unaojumuisha wapiganaji wa makundi mbalimbali ya nchini Yemen, wanajaribu kuirejesha serikali inayotambuliwa kimataifa iliyondolewa madarakani mwaka 2014 na waasi wa Houthi wanaoungwa mkonona Iran.

Amnesty international Logo
Nembo ya shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty InternationalPicha: picture-alliance/dpa/S.Kahnert

Taarifa ya shirika hilo la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International imesema, wanajeshi wa Umoja wa falme za kiarabu wanapokea silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola kutoka kwa mataifa ya Magharibi na mataifa mengine lakini silaha hizo hupitishwa kisiri kwa makundi ya waasi nchini Yemen yanayojulikana kufanya uhalifu wa kivita.

Imeongeza kuwa kuenea kwa makundi ya wapiganaji kunazidisha hali ya hatari kwa  wananchi wa Yemen ambao tayari maelfu kwa maelfu wameshauwawa kutokana na vita huku mamilioni wakiwa katika hatari ya kukabiliwa na njaa. Hata hivyo serikali ya Umoja wa Falme za kiarabu haikujibu mara moja ombi la kutaka maoni juu ya taarifa hiyo ya Amnesty International.

Nchi hiyo ya kifalme tayari imeshatoa mafunzo na kuwapa silaha maelfu ya wapiganaji wa Yemen wengi wakiwa katika mikoa ya kusini na maeneo ya pwani ya Magharibi kama sehemu ya wanajeshi au vikosi vinavyopambana na waasi wa Houthi wanaodhibiti maeneo mengi ya miji ukiwemo mji mkuu Sanaa pamoja na mji wa bandari wa Hodeidah unaotumiwa kama njia ya kupitishia msaada wa kibinadamu.

Jamii ya Kimataifa yashinika yatoa wito wa kumalizika vita vya miaka minne Yemen

Mataifa ya Magharibi, mengi ambayo yalitoa silaha na huduma za kijasusi kwa muungano huo, yanaendelea kushinikiza kumalizika vita hivyo vya Yemen vya takriban miaka minne nchini Yemen, hasa baada ya mauaji ya mwaandishi habari wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi yalioongeza uchunguzi wa shughuli za Saudi Arabia katika eneo.

Jemen | Bewaffnete Sympathisanten der Huthi-Rebellen
Baadhi ya wapiganaji wa YemenPicha: Getty Images/AFP/M. Huwais

Hata hivyo makundi ya kutetea haki za binaadamu yamezishutumu pande zote kufanya uhalifu wa kivita ikiwa ni pamoja na mateso kwa wafungwa, madai ambayo yamekanushwa na pande zote. Amnesty International imetoa wito kwa mataifa kusimamisha uuzaji wa silaha kwa pande zinazohasimiana hadi pale kutakapomalizika kitisho cha uvunjifu wa haki za binaadamu au hata sheria ya haki za binaadamu.

Mgogoro huo wa Yemen unaonekana kama vita vya chini kwa chini kati ya waislamu wa madhehebu ya Sunni wakiongozwa na Saudi Arabia na wale wa kishia wanaoongozwa na Iran. Waasi wa Houthi wamekanusha madai ya kupokea silaha kutoka kwa Iran wakisema vita vyao ni dhidi ya rushwa.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters

Mhariri:  Gakuba, Daniel