AMMAN: Mfalme Abdulla aitaka Marekani iongeze juhudi za upatanishi | Habari za Ulimwengu | DW | 21.02.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

AMMAN: Mfalme Abdulla aitaka Marekani iongeze juhudi za upatanishi

Mfalme Abdulla II wa Jordan ameitolea mwito Marekani iongeze juhudi zake za upatanishi kusaidia kufikiwa kwa mkataba wa amani kati ya Israel na Palestina unaokabiliwa na kitisho cha kuundwa kwa serikali ya umoja wa taifa ya mamlaka ya Palestina.

Mfalme Abdullah aliyasema hayo jana baada ya kukutana na waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice na rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, katika mikutano tofauti mjini Amman.

Mfalme huyo alisema jukumu la Marekani ni muhimu katika kuzipiga jeki juhudi za upatanishi na kuvishinda vikwazo vinavyozuia kufikiwa kuundwa kwa mataifa mawili ya Israel na Palestina.

Wakati huo huo, chama kikubwa zaidi cha kisiasa nchini Jordan, Islamic Action Front, kimeihimiza serikali ya Jordan ikatae kile ilichokiita juhudi za Marekani kutaka kuyavuruga makubaliano yaliyofikiwa na vyama vya Hamas na Fatah kwenye mkutano wa mjini Makkah Saudi Arabia mapema mwezi huu.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com