1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amano ameidhinishwa kumrithi ElBaradei

14 Septemba 2009

Shirika la kimataifa la nishati ya nyuklia IAEA leo limemuidhinisha rasmi Yukiya Amano wa Japan kuwa mkurugenzi mkuu mpya wa shirika hilo kuanzia tarehe mosi Desemba.

https://p.dw.com/p/Jf3D
The designated director general of International Atomic Energy Agency (IAEA), Japan's Yukiya Amano, delivers a speech at the beginning of a general confernce of the IAEA, at Vienna's International Center, in Vienna, Austria, on Monday, Sept. 14, 2009. (AP Photo/Ronald Zak)
Mkurugenzi Mkuu mteule wa IAEA, Yukiya Amano.Picha: AP

Amano anamrithi Mohamed El Baradei anaeondoka mwisho wa mwezi wa Novemba baada ya kushika wadhifa huo kwa miaka 12. Amano alikwishachaguliwa na bodi la magavana 35 wa IAEA tangu mwezi wa Julai lakini uteuzi wake umehitaji kuidhinishwa rasmi na nchi wanachama 150 katika mkutano wake wa mwaka. Muda mfupi baada ya kuidhinishwa, Amano katika hotuba yake alisisitiza umuhimu wa kuwepo uwiano katika dhima mbili za shirika hilo kuhusika na nishati ya nyuklia na kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia. Amesema,usambazaji wa silaha za nyuklia na hatari ya silaha hizo kuangukia mikononi mwa magaidi ni kitisho kinachozidi kuikabili jumuiya ya kimataifa kwa sababu ujuzi na teknolojia yake inaweza kusambazwa kwa urahisi. Wakati huo huo alimsifu mtangulizi wake ElBaradei kwa kupigania amani bila ya kuchoka. Amesema atakumbukwa kwa yale aliyofanikiwa kutekeleza wakati wa muhula wake wa miaka 12.

ElBaradei mwenye miaka 67 mara kwa mara amekosolewa hasa na Marekani kwamba hakuwa na msimamo mkali zaidi kuelekea Iran.Nchi hiyo inashukiwa kuwa mradi wake wa nishati ya nyuklia unatumiwa kutengeneza bomu la atomiki kwa siri. El Baradei hii leo alipoufungua mkutano wa mwaka mjini Vienna, alilihimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuipatia IAEA mamlaka zaidi ya kuzuia usambazaji wa teknolojia ya bomu la atomu badala ya kutegemea vikwazo visivyosaidia mara nyingi. Bila shaka hapo alidhamiria Iran inayoendelea na mradi wake wa kurutubisha madini ya uranium licha ya kuwekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa.

Lakini juma lililopita, Iran inayopuuza vitisho vya kuwekewa vikwazo vikali zaidi, iliwasilisha mapendekezo ya kujadili jitahada za kupunguza silaha za nyuklia kote duniani pamoja na mada zingine za kimataifa lakini haitojadili mradi wake wa nyuklia. El Baradei ameipongeza Marekani kwa kuwa tayari kufufua majadiliano pamoja na Iran bila ya kuiwekea masharti. Wakati huo huo ameonya kuwa haitosaidia kutoa vitisho vya kuiwekea Iran vikwazo vikali zaidi ikiwa mazungumzo hayo hayatofanya maendeleo. Kwa upande mwingine, msemaji wa Javier Solana, mwakilishi mkuu wa sera za nje za Umoja wa Ulaya, leo hii mjini Brussels amethibitisha kuwa Solana na wajumbe wa nchi wanachama watano yaani Uingereza, Ufaransa,China,Marekani na Urusi zenye kura turufu katika Baraza la Usalama pamoja na Ujerumani watakutana na mpatanishi wa Iran Saeed Jalili tarehe mosi mwezi wa Oktoba. Solana tangu mwaka 2006 anajaribu kuileta Iran katika meza ya majadiliano pamoja na nchi za magharibi kuujadili mradi wake wa nyuklia.

Mwandishi: P.Martin/AFPE/RTRE

Mhariri: M-Abdul-Rahman