Althaus aongoza orodha ya CDU jimboni Thüringen | Magazetini | DW | 16.03.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Althaus aongoza orodha ya CDU jimboni Thüringen

Waziri mkuu aliyejeruhiwa ateuliwa kuongoza orodha ya watetezi wa chama chake kwaajili ya uchaguzi ujao jimboni mwake

default

Thüringen yajiandaa kwa uchaguziWahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha zaidi na kuteuliwa waziri mkuu wa jimbo la Thüringen, Dieter Althaus, kuongoza orodha ya uchaguzi wa jimbo kwa tikiti ya chama cha CDU, na mapendekezo mepya ya kiongozi wa chama cha CSU, Horst Seehofer, kutaka kodi ziada ipunguzwe .


Kuhusu kuteuliwa Althaus limeandika gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG:


"Kawaida maneno ya wanasiasa yanachosha kuyasikiliza. Ni sawa na makadirio ya hali mbaya ya hewa. Na kuna wakati ambapo mtu unahisi maneno hayo hayavumiliki kabisa. Na hali hiyo ndiyo iliyojitokeza wakati wa mkutano mkuu wa tawi la chama cha CDU katika jimbo la Thüringen uliotishwa mwishoni mwa wiki. Wiki 11 baada ya ajali katika milima ya theluji, ambapo bibi mmoja mwenye umri wa miaka 41, Beata Christiandl, alifariki dunia,wana CDU wamemteuwa Dieter Althaus, bila ya kuwepo mkutanoni, aongoze orodha ya watetezi wao katika uchaguzi wa jimbo-na marafiki zake chamani wanafanya kana kwamba hakuna kilichojiri. Hata hivyo, kiini macho hicho hakimhadai yeyote;hakuna asiyejua kwamba Althaus amegeuka mzigo ambao hawajui jinsi ya kuutua.


Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG linahisi wana CDU wa THÜRINGEN hawakua na chaguo jengine...


"Wangefanya nini chengine, kama si kumuunga mkono Althaus? Ingawa kulikua na wengine wawili au hata watatu ambao wangeweza kuorodheshwa baada ya Althaus, hata kama hakuna bado anaewajua,hata hivyo, wakati wao bado haujawadia-hasa kwa sababu ya ile hali kwamba hakuna anaethubutu kusema chochote tangu mwenyewe waziri mkuu alipofikwa na ajali."


"Gazeti la NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG linajishughulisha na kilichosemwa na mwenyekiti wa chama cha CSU kuhusu kodi ziada. Gazeti linaendelea kuandika:


Horst Seehofer anabidi afikirie jengine. Mapendekezo yake ya kila wakati kutaka kodi ziada kwa makampuni na mashirika fulani ipunguzwe haraka hayavutii hata kidogo.Kwa sababau si jambo linaloingia akilini kutia njiani marekebiso kama hayo kabla ya uchaguzi mkuu kuitishwa. Huo ndio msimamo wa kansela na chama chake cha CDU. Na wana social Democratic wana maoni sawa na hayo.Kutokana na kunung'unika kila kwa mara dhidi ya siasa ya serikali ya muungano, kiongozi wa CSU anautia ila uongozi wa kansela.


Gazeti la Der TAGESPIEGEL la mjini Berlin linasema ingekua bora zaidi kama kodi hiyo ingepandishwa.Gazeti linaebndelea kuandika:


La maana zaidi ni kupandisha kodi. Bila shaka, sio sasa, katika kipindi hiki cha kuzorota shughuli za kiuchumi. Lakini baadae.Kwa sababu mabilioni ya fedha kwa ajili ya kuzinusuru benki, na mipango miwili ya kuinua uchumi na kugharamia ajira ya muda mfupi,tunalipa sisi kupitia kodi za mapato.Kwa sasa kila la kufanya lifanywe kuumaliza mgogoro wa kiuchumi unaotishia kuzidisha idadi ya wasiokua na ajira ambao watalazimika kutegemea msaada wa huduma za jamii.


Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/DPA

Mhariri: Miraji Othman


 • Tarehe 16.03.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HCsD
 • Tarehe 16.03.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HCsD
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com