Aliyevunja turathi Timbuktu ahukumiwa | Magazetini | DW | 30.09.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani

Aliyevunja turathi Timbuktu ahukumiwa

Hukmu ya korti ya mjini The Hague dhidi ya kuvunjwa turathi za tamaduni za kimataifa mjini Timbuktu,ughali wa maisha nchini NIgeria na elimu bure nchini Afrika Kusini ni miongoni mwa mada za Afrika Magazetini wiki hiii

Ahmad Al Faqi Al Mahdi Prozess Den Haag Strafgerichtshof Weltkulturerbe (picture-alliance/dpa/P.Post)

Ahmad Al Faqi akisikiliza hukmu yake mjini The Hague

Tuanzie lakini moja kwa moja katika njia panda inayoiunganisha korti ya kimataifa ya uhalifu mjini The Hague na mji wa kaskazini mwa Mali-Timbuktu.Takriban magazeti yote ya Ujerumani yamezungumzia hukmu iliyotolewa na korti ya mjini The Hague dhidi ya Ahmad al-Faqi al-Mahdi aliyehukumiwa kifungo cha miaka tisa jela kwa makosa ya uhalifu wa vita kwasababu ya kuhusika na kubomolewa mwaka 2012 majengo 10 ya kihistoria katika mji wa jangwaani wa Timbuktu. Gazeti la kusini mwa Ujerumani "Süddeutsache Zeitung" linakumbusha kwamba adhabu hiyo si kubwa kwasabu ,kesi hiyo ilipoanza tu,mtuhumiwa huyo alifikia makubaliano pamoja na upande wa mashtaka na kukiri makosa yake ili badala yake apunguziwe  makali ya adhabu dhidi yake.

Mwongozo wa korti ya kimataifa ya uhalifu unaweka wazi kabisa kwamba mhukumiwa huyo,mfuasi wa itikadi kali atafungwa katika nchi mojawaapo kati ya 124 zilizotia saini makubaliano ya kuundwa korti hiyo na sio mjini The Hague na kwamba ataachiwa huru baada ya kutumikia thuluthi mbili ya kifungo chake jela. Kwa maneno mengine al Mahdi ataachiwa huru baada ya miaka sita. Na muda alioupitisha jela mjini The Hague tangu septemba mwaka 2015,kabla ya kesi kuanza,nao pia  utahesabiwa na kupunguzwa. Hii ni mara ya kwanza linaandika gazeti la Süddeutsche" kwa korti ya kimataifa kujishughulisha na kesi ya kubomolewa majengo ya turathi za tamaduni ya kimataifa-kitendo kinacholinganishwa na uhalifu wa vita. Gazeti la Süddeutsche limelinukuu shirika la haki za binaadam Human Rights Watch likiitaja hukmu hiyo kuwa ni onyo dhidi ya kuteketezwa turathi za kihistoria.

Wabakabaji na Watesaji pia waandamwe

Gazeti la mjini Berlin-Berliner Zeitung linaitaja hukmu hiyo kuwa ni onyo kwa wafuasi wa itikadi kali wanaoteketeza majengo ya kihistoria nchini Afghanaistan,Iraq na Syria. Berliner Zeitung linalinukuu shirika la haki za binaadam Amnesty International lililotoa wito wa kuandamwa pia wahalifu wanaoahusika na mauwaji,ubakaji na mateso katika eneo la kaskazini mwa Mali.

Ughali wa Maisha Nigeria

Mada nyengine ya Afrika iliyopewa umuhimu na wahariri wa magazeti ya Ujerumani wiki hii inahusu ughali wa maisha nchini Nigeria. Gazeti la Handelsblatt linasema hakuna nchi yoyote ya Afrika ambako pengo linalotenganisha mahitaji na ukweli wa mambo ni kubwa kama Nigeria-nchi yenye wakaazi wengi zaidi barani Afrika kutokana na wakaazi wake milioni 175.Tangu nchi hiyo ilipotangazwa kuwa dola kubwa zaidi la kiuchumi barani Afrika miaka mitatu iliyopita,nchi hiyo inayochimba mafuta ilivamiwa na kuzongwa na washauri wa wajasiria mali. Lakini kuporomoka bei ya mafuta na kushindwa nchi hiyo kwa miaka kadhaa sasa kuufanyia marekebisho mfumo wake wa kiuchumi bila ya kutegemea mafuta,vimepelekea shughuli za uchumi kupooza.

Baada ya ukuaji wa kiuchumi wa karibu asili mia 7 mwaka 2014,shirika la fedha la kimataifa linakadiria  kiwango hicho kitapungua na kusalia asili mia mbili tu mwaka huu. Kutokana na hali mbaya ya kiuchumi Handelsblatt linasema serikali mpya ya jenerali wa zamani Muhammadu Buhari iliyoingia madarakani mwaka jana imeahidi kuhimiza shughuli za kiuchumi katika sekta nyenginezo. Serikali hiyo inapanga kuwekeza katika shughuli za kilimo na miundo mbinu. Juhudi za kujikwamua toka mfumo wa uchumi unaotegemea mafuta zinakabiliwa na kishindo cha ughali wa maisha unaofikia asili mia 20 na vurugu za kisiasa. Mahitaji mi makubwa linasema gazeti hilo la masuala ya kiuchumi linalozungumzia pia shiza za nishati katika nchi hiyo yenye kuchimba mafuta barani Afrika.

 Hatima ya Elimu bure haijulikani Afrika Kusini

Na hatimae gazeti la Neues Deutschland limezungumzia kutoweka ndoto ya wanafunzi wa Afrika Kusini kupata elimu bure baada ya malipo hayo kuongezeka na kusababisha wanafunzi kulalamika majiani. Serikali inapanga kupitisha auamuzi wake wa mwisho mwezi huu wa October.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/All Presse

Mhariri:Yusuf Saumu