1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Shabaab wavamia, wauwa polisi Kenya

26 Mei 2015

Maafisa 13 wa polisi nchini Kenya hawajulikani walipo na wengine watano wakiwa wamejeruhiwa baada ya kundi la al-Shabaab kuyavamia na kuyachoma moto magari matano ya polisi usiku wa Jumatatu.

https://p.dw.com/p/1FWWN
Garissa Kenia Soldaten
Picha: picture-alliance/dpa

Msemaji mkuu wa kikosi cha polisi George Kinoti amelithibitishia shrika la habari la AP kwamba maafisa 13 hawajulikani walipo baada ya mashambulizi hayo yaliyotokea kaskazini mashariki ya Kenya karibu na mpaka wa Somalia . Lakini taarifa iliyosainiwa na Mkuu wa Polisi J.K Boinnet imesema maafisa wawili wapo katika hali mbaya na watatu wamepata majeraha ya wastani bila ya kutaja kuwa kuna wengine 13 wasiojulikana mahala walipo.

George Kinoti ameeleza kwamba kikosi cha polisi kimepelekwa katika eneo hilo ili kuwatafuta mafisa hao waliopotea pamoja na waliohusika na mashambulizi hayo.

Afisa wa polisi aliyekataa kujitambulisha kwa jina, ameliambia shirika la habari la dpa wanamgambo hao wa al-shabab wameyaripuwa magari manne ya vikosi vya usalama vya Kenya yaliyokuwa yakieleka katika kijiji cha Yumbis mjini Garissa, Kaskazini Mashariki ya Kenya.

al-Shabaab Kämpfer in Somalia
Picha: picture alliance / AP Photo

"Bado hakuna hakika watu wangapi wameuliwa katika mashambulizi hayo…na kuwa wengine kadhaa bado hawajulikani walipo," amesema afisa huyo.

Afisa huyo aliongeza kwa kusema, maafisa hao wasiotambulika mahala walipo walikuwa kati ya kikosi cha polisi 20 kilichokuwa kikirudi kuchukua bunduki iliyosahauliwa na afisa mmoja wakati gari zao ziliposhambuliwa na wanamgambo wa Al-shabab.

Shambulizi hilo limefanyika wiki moja baada ya wanamgambo wa kundi la al-shabab kuvivamia vijiji vya Yumbis, Welmareer pamoja na Damajale katika wilaya ya Garissa, lakini walizuwiwa na jeshi pamoja na kikosi cha polisi.

Wanamgambo hao ingawaje walirudi tena Yumbis Jumatatu usiku na kukidhibiti kijiji hicho.

Al-shabab kukiri kuhusika na shambulizi

Kundi la al-shabab limedai kuhusika na shambulizi hilo. "Wapiganaji wetu wamefanikiwa kuwauwa zaidi ya maafisa wa polisi 20. Pamoja na kuharibu magari matano ya polisi wakati wa shambulizi letu," amesema msemaji mkuu wa kundi la al-shabab Sheikh Abdiasis Abu Musab alipokuwa akizungumza na kituo cha redio cha Andalus kinachounga mkono upande wa uasi.

Jeshi la Kenya limesema leo kuwa limefanikiwa kuwauwa wanamgambo saba wa kundi la Al-shabab ndani ya Somalia.

Al-shabab pia wamekiri kuhusika na shambulizi la mauwaji ya wanafunzi 148 katika chuo kikuu cha mji wa Garissa, wezi uliopita, pamoja na shambulizi la mwaka 2013 la jengo la biashara la Westgate ambapo takriban watu 67 waliuwawa.

Al-shabab imekuwa ikifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika maeneo ya Kenya yaliyo karibu na mpaka wa Somalia, huku ikidai lazima vikosi vya Kenya viondoke nchini Somalia.

Mwandishi:Yusra Buwayhid/APE/DPAE/AFP

Mhariri:Josephat Charo