al-Maliki kukutana na Obama leo | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.07.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

al-Maliki kukutana na Obama leo

Waziri Mkuu wa Iraq Nouri al-Maliki anatarajiwa kukutana na Rais Barack Obama wa Marekani huko Washington baadae leo

default

Waziri Mkuu wa Iraq Nouri al-Maliki

Watu wanane wamefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa vibaya baada ya kutokea miripuko ya mabomu katika jiji la Baghdad na Maeneo ya Magharibi mwa jiji hilo.Tukio hili linatokea ukiwa umebaki muda mfupi kabla ya Waziri Mkuu wa Iraq Nouri Al-Maliki akutane na Rais Barack Obama wa Marekani huko Washington.

Mashambulio hayo yanatokea wakati ambapo Waziri Mkuu, Nouri al-Maliki, yupo nchini Marekani,ikiwa ziara ya kwanza ya kikazi kwa kiongozi huyo tangu Rais Obama aingie madarakani.

Aidha mkutano huo unafanyika ikiwa wiki tatu tu zimepita tangu wanajeshi wa Marekani wajiondoe katika jiji la Baghdad na miji mingine nchini humo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ujerumani, DPA, mripuko mkubwa ulitokea katika mji ulio karibu na Baghadad wa Sadr na kusababisha vifo vya watu 5 na wengine 13 kujeruhiwa.

Mripukio huo ulilenga mafundi ujenzi waliokuwa katika eneo la ujenzi wakisubiri kuajiriwa kwa siku ya leo.

Muda mfupi baadae, miripuko mingine miwili mfululizo ilitokea katika ilitokea katika makutano ya barabara katikati ya jiji la Baghdad, karibu na maeneo ya Karada na Makat na kujeruhi watu 10.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi nchini Iraq limesema katika mji wa Ramadi, ulio umbali wa Kilometa 120 mashariki mwa Baghadad, polisi imewazuia watu wasitoke nje baada ya kutokea mripuko wa bomu katika gari moja na kusababisha watu watatu kupoteza maisha na wengine zaidi ya 19 kujeruhiwa.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchi hiyo, vinasema kuwa mtu asiyefahamika aliegesha gari yake karibu na hoteli moja ambayo muda mfupi baadae iliripuka.

Uchunguzi wa Polisi umebaini kuwa kuna gari nyingie iliokuwa karibu na gari lililoripuka, ikiwa na bomu ambapo, hata hivyo, uchunguzi wa kina unaendelea.

Huko katika mji wa al-Sadr, jeshi la Iraq limewatia mbaroni watu wanne wakiwa wa silaha pamoja na pasi za kusafiria za Kisiria.

Sambamba na hali ilivyo hiki karibuni Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Roberts Gates, anasema kiwango cha ushirikiano na Vikosi vya Usalama nchini Iraq kinaendelea kuwa kizuri zaidi ya inayoripotiwa katika vyombo vya habari.

Katika ziara ya leo ya Waziri Mkuu Nouri al-Malik pamoja na kutafuta ushirika katika sekta ya uwekezaji nchini Marekani atagusia suala la ulinzi nchini mwake.

Afisa wa Baraza la Mawaziri la Iraq, Alli al Mousawi, amesema Maliki ameondoka jana asubuhi nchini humo akimbatana na Mawaziri wa Ulinzi na Mambo ya Ndani pamoja na Mkuu wa Kamati ya Uwekezaji.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Robert Gibbs, amesema Obama atakutana na al-Maliki leo.

Amesema pamoja na mambo mengine, mjadala mkubwa leo hii utakuwa juu ya hali ya kisiasa nchini ambayo itawezesha kuleta maendeleo nchini Iraq baada miaka mingi ya vita.


Mwandishi: Sudi Mnette DPA

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 22.07.2009
 • Mwandishi Eva Klaue-Machangu
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Iv8L
 • Tarehe 22.07.2009
 • Mwandishi Eva Klaue-Machangu
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Iv8L
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com